Kutimia au Kubatilika kwa Unabii;

 


JE, UNABII UNAWEZA KUBATILIKA? (JE BIBLIA INATUAMBIA NINI JUU YA KUBATILIKA AU KITIMIA KWA UNABII?)


Bwana Yesu asifiwe sana mtu wa Mungu!

Nashukuru sana Mungu kwa kunipa kibali siku ya leo kukutana nawe tena katika makala hii kwa nia ya kujifunza zaidi juu ya mambo yahusuyo "Unabii."

Najua unaweza ukajiuliza, kwa nini tujifunze mambo kadhaa kuhusu unabii?
Lakini inawezekana huamini katika unabii, na hivyo si jambo muhimu wewe kujua kuhusu mada hii.
Au pia, kwa imani yako unaamini nyakati hizi hakuna manabii.

Jambo moja ninalotaka kukuambia ni kwamba, naelewa na ninaheshimu mtazamo wako na mawazo yako juu ya hicho unachokiamini.

Lakini ningependa ufahamu kwamba kuna ukweli ambao huujui kuhusiana na mada hii, ukweli ambao ukiufahamu utaondokana kabisa na mtazamo ulio nao.
Bwana Yesu asifiwe sana!

Sasa ili unielewe vizuri, natamani tukae chini kama watu wanaojifunza Neno la Mungu, tufungue akili zetu, na tujadili kwa pamoja huku tukiangalia Maandiko Matakatifu yanasemaje juu ya mada hii ambayo imekuwa ikileta mkanganyiko mkubwa sana kwenye makanisa na huduma mbalimbali.

Bila shaka, sote tumewahi kuona au kusikia mtu akitolewa unabii—labda kuhusu maisha yake, ndoa, uchumi, au huduma yake. Wakati mwingine unabii ule unatimia haraka sana, lakini wakati mwingine miaka inapita na hakuna kitu kinachotokea.

Sasa hapo ndipo watu wengi huanza kujiuliza maswali:
Je, unabii unaweza kubatilika?
Je, Mungu ni muongo hata kubadilisha alichonena?
Na wengine huona kama mjumbe aliyeleta ujumbe pengine alileta ujumbe kwa mtazamo wake na si ujumbe halisi wa Mungu.

Kabla hatujajibu kwa nini unabii unatimia au kubatilika, hebu kwanza tuweke msingi wa darasa letu kwa kuelewa maana ya nabii na unabii kwa mujibu wa Maandiko Matakatifu.

    UTANGULIZI:

KUELEWA MSINGI WA UNABII NA NABII

1. Nabii ni Nani?

Nabii ni mtu anayechaguliwa na Mungu kuwa msemaji wa Mungu kwa watu wake.

Kwa mujibu wa Biblia, nabii ni mtu anayenena kwa niaba ya Mungu kwa watu.

Tukisoma habari za kuteuliwa kwa Musa pamoja na Haruni kuwa viongozi wa wana wa Israeli, tunaona Mungu alimfanya Musa kuwa kama Mungu kwa Farao na Haruni ndugu yake kuwa nabii wake. Ukumbuke Musa awali alimwambia Mungu, "Mimi si mjuzi wa kusema," ndipo Mungu akamteulia Haruni.
Andiko hili linapatikana katika kitabu cha Kutoka 7:1, ambapo Mungu alimwambia Musa:

"Tazama, nimekufanya wewe kuwa Mungu kwa Farao; na Haruni ndugu yako atakuwa nabii wako."
 Bwana Yesu asifiwe;

Kwa maana nyingine, kama Mungu alimfanya Musa kuwa Mungu kwa Farao na Haruni nduguye kuwa ndiye nabii, yaani mzungumzaji wa ujumbe atakaotumwa na Musa, hapa tunaona wazi kuwa nabii yeye ni kama kinywa cha kupeleka ujumbe wa Mungu kwa watu.

Kwa maana hiyo tunaweza kusema:
Nabii ni mtu aliyeitwa na Mungu kupokea na kuwasilisha ujumbe.

Ujumbe huo unaweza kuwa wa:
- Kuonya watu.
- Kuwataka watu watubu juu ya uovu fulani.
- Kufundisha yale Mungu anayotaka wao wayafahamu.
- Kuwafariji watu wa Mungu.
- Kufunua mambo yajayo pale Mungu anapotaka kufanya hivyo.

Tunaweza kupata mifano kadhaa hapa ili kukufanya uelewe zaidi:

- Nabii Nathani alitumwa kumkemea Daudi baada ya dhambi yake. Na ule ujumbe ulimfanya Daudi akabadilika na kutubu. (2 Samwel 12: 1-15)
- Nabii Yona alitumwa kuonya Ninawi hata hivyo watu wa Ninawi walitubu na MUNGU alighairi hukumu iliyokuwa iwapate.
- Nabii Isaya alitoa maonyo, kwa taifa la Yuda, mafundisho na unabii kuhusu kuhusu ujio wa Masihi.(Isaya 1:2-20; 7:14; 9:6-7; 53:1-12)

Kwa hiyo mpaka sasa kama ulikuwa unapinga kuwa haiwezekani kuwapo na manabii siku hizi, nadhani tunaweza kuwa tunazungumza lugha moja kuwa manabii wapo. Ili ujue wapo, turejee tena maana ya nabii ni nini:

"Nabii ni mtu aliyeitwa na Mungu kuwa msemaji wake kwa wanadamu."

Katika Kutoka 7:1: tunaona imeandikwa,
"BWANA akamwambia Musa, Tazama, nimekufanya wewe kuwa Mungu kwa Farao; na Haruni ndugu yako atakuwa nabii wako."

Hapa neno "nabii wako" lina maana ya "msemaji wako."

Kwa hiyo, nabii wa Mungu ni msemaji wa Mungu.

Sasa nikuulize maswali kadhaa, ndugu yangu katika Bwana, nawe unisaidie kufikiri pamoja nami:

Je, Mungu hana wasemaji wake nyakati hizi hapa duniani?

Kwa hiyo Mungu akitaka kuzungumza na wanadamu huwa anatumia viumbe gani kusema na watu wake?

Wakati unatafakari hayo, naomba nikurejeshe katika Neno la Mungu, kutoka kitabu cha Amosi 3:7, linavyosema:

Naomba kunukuu:
"Hakika Bwana MUNGU hatafanya neno lo lote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake."

Bwana Yesu asifiwe sana!

Bila shaka unaendelea kujua ukweli fulani na kuelewa hatua kwa hatua juu ya uwepo wa unabii na manabii.

Lakini kama maswali hayo hapo juu hayatoshi, nikuulize swali tena.

Kama nabii ni msemaji wa Mungu hapa duniani, je, huwa watu wanaotupasha habari za Mungu hapa duniani na kutueleza mambo yatakayotokea, kisha yakatokea, hao tutawaitaje?

Bila shaka sasa umepata majibu.

Lakini natamani tuelewe kuwa nabii si mtabiri wa nyota, mpiga ramli au mwenye uwezo wa kutambua mambo yajayo na kubashiri juu ya yajayo. Hapana, msingi wa unabii haujengwi katika hayo.

Na wanaofanya hivyo wana agenda zao nyingine ambazo si agenda za kumtumikia Mungu aliye hai. Pengine wanafanya wasichokijua au wanatumikia ufalme mwingine kabisa kwa kujua au kwa kupokea kutoka kwa viongozi wao bila wao kujua.

MUNGU AKITUPA KIBALI WAKATI MWINGINE TUTAJIFUNZA NAMNA YA KUMTOFAUTISHA MTUMISHI SAHIHI WA MUNGU NA MTUMISHI ASIYEMTUMIKIA MUNGU NA HAPO TUTAJIFUNZA KWA KINA KUHUSU UWEPO WA MANABII WASIO WAAMINIFU KWA MUNGU INGAWA WAKATI MWINGINE WANATABIRI NA MAMBO HUTOKEA.

2. Unabii ni Nini?

Unabii ni ujumbe wa Mungu unaoletwa kwa wanadamu kupitia nabii.

Kwa lugha rahisi na ya kimaandiko, unabii ni Mungu akizungumza na wanadamu kupitia chombo alichokichagua.

Katika 2 Petro 1:21:

"Maana unabii haukuletwa po pote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu."

Kwa hiyo kila unapokutana na unabii wa kweli, chanzo chake si akili ya mwanadamu wala hisia zake, bali ni Roho Mtakatifu anayefunua mapenzi ya Mungu.

Au:

"Unabii ni ufunuo wa jambo fulani, au makusudi, au ujumbe wa Mungu kwa wanadamu, unaotolewa kupitia mtu aliyechaguliwa na Mungu, anayeongozwa na Roho Mtakatifu kwa ajili ya kujenga, kuonya, kufariji, kuelekeza au kufunua yale ambayo Mungu anataka watu wake wajue."

AINA ZA UNABII KWA MUJIBU WA BIBLIA

Ili uelewe kwa nini unabii unatimia au la, lazima ujue kuwa unabii haufanani.

Biblia inatuonyesha aina kadhaa za unabii.

Mimi nimejaribu kuugawa katika makundi matatu:

1. Unabii wa Kujenga, Kufariji na Kuonya (Ujumbe wa Wakati Uliopo).

Huu ni unabii unaotolewa ili kurekebisha tabia, kutia moyo, kuonya au kujenga watu wa Mungu.

1 Wakorintho 14:3 inasema:

"Bali yeye afanyaye unabii husema na watu maneno ya kuwajenga, na kuwafariji, na kuwatia moyo."

Kwa hiyo kumbe unabii ni pamoja na kuwajenga watu, yaani kuhakikisha wanakuwa katika msingi imara kwa Kristo, ambapo hapo hapo kuna maonyo dhidi ya mambo yanayomchukiza Mungu, na kutiwa moyo, na hata kuwafariji wanapokuwa katika hali inayohitaji faraja.

Lakini kumbuka, hayo yote hutendeka kwa uwezo wa Mungu na Roho Mtakatifu akiyafunua yale Mungu anayotaka yatendeke.

Bwana Yesu asifiwe sana!

Hiyo ndiyo aina ya kwanza ya unabii.

Aina nyingine ya unabii ni:

2. Unabii wa Matukio ya Baadaye (Predictive Prophecy)

Huu ni unabii unaotangaza jambo ambalo bado halijatokea, lakini litatokea katika siku zijazo.

Mfano mzuri ni unabii wa Isaya kuhusu kuzaliwa kwa Yesu Kristo mamia ya miaka kabla ya kutimia kwake.

Hata katika maisha ya kawaida, watumishi wa Mungu, manabii, wanaweza kufunuliwa mambo yatakayotokea katika dunia hii, na kwa kweli wakati mwingine yanatokea na kuleta udhihirisho.

Mungu anaweza kumtumia nabii wake kueleza juu ya hali ya hatari katika nchi fulani au utawala fulani, na namna mambo yanavyohitajika kurekebishwa, na kwamba kama yasipotazamwa na kurekebishwa, inakuwa kama ilivyonenwa.

Aina nyingine ya unabii ni:

3. Unabii Wenye Masharti (Conditional Prophecy)

Huu ni unabii ambao utimilifu wake unahusiana na mwitikio wa mwanadamu mbele za Mungu.

Mungu mwenyewe anaeleza kanuni hii katika Yeremia 18:7–10. Mtu au taifa linaweza kutubu, likapata rehema; au likaasi, likakosa baraka zilizokuwa zimekusudiwa.

Naomba kunukuu kutoka katika kitabu cha Nabii Yeremia 18:7–10:

«7 "Wakati wo wote nitakaposema katika habari za taifa, na katika habari za ufalme, ya kwamba nitang'oa, na kubomoa, na kuangamiza;

8 ikiwa taifa lile nililolinenea litageuka, na kuacha uovu wake, basi nitalighairi lile baya nililodhamiria kulitenda.

9 Na wakati wo wote nitakaposema katika habari za taifa, na katika habari za ufalme, ya kwamba nitalijenga na kulipanda;

10 ikiwa likifanya yaliyo mabaya machoni pangu, hata lisitii sauti yangu, basi nitatubu kwa habari ya mema yale ambayo nilisema ya kwamba nitalitendea."»

(Mwisho wa kunukuu.)

Kwa andiko hilo utaona wazi, pasi na shaka, kuwa unabii unaweza kubatilika kwa sababu ya kutii au kutotii kwa mlengwa (anayehusika na unabii huo, au walengwa wa unabii huo).

Unaweza ukapewa ujumbe wa Mungu kuwa unahitajika kuwa, pengine, kiongozi katika taasisi fulani, lakini wewe baada ya muda ukabadilisha mwelekeo. Wakati mwingine hata ukawa unaomba maombi yanayobatilisha unabii ule.

Labda unaomba uhamishwe kutoka taasisi hiyo na uhamie ofisi nyingine kwa sababu taasisi uliyopo haikulipi vizuri. Kwa kuwa unamuomba Mungu akuhamishe kutoka taasisi hiyo uliyopo na uliyotabiriwa kuwa utakuwa kiongozi hapo, naye Mungu anaweza kukujibu kwa kadiri unavyoomba, maana hukumwuliza Mungu juu ya uamuzi wako huo, ila uliona vema kutenda kwa mashauri yako mwenyewe.

Matokeo ya maombi yako yanaweza kufanya usiuone utimilifu wa unabii wa awali kuwa utakuwa kiongozi katika taasisi uliyokuwa.

Bwana Yesu asifiwe!

Nafikiri unanielewa, mwana wa Mungu.

    JINSI YA KUPIMA UNABII

Mtu wa Mungu, kabla hatujaendelea mbele, kuna jambo muhimu sana ambalo Biblia inalitilia mkazo.

Sio kila neno linaloitwa unabii linapaswa kukubaliwa moja kwa moja bila kulichunguza.

Mtume Paulo anatuagiza katika 1 Wathesalonike 5:20–21:

"Msiudharau unabii; jaribuni mambo yote; lishikeni lililo jema."

Tunachojifunza hapa ni nini?

Kwanza, tusiudharau unabii.

Pili, kila jambo lazima lipimwe katika msingi wa Neno la Mungu.

Huwa napenda kuwaambia watu kuwa kama wewe ni mwokovu na huwezi, au huna desturi ya kusoma Neno la Mungu, ni sawa na mtu anayeamini asichokijua.
Madhara yake ni kwamba unakuwa Mkristo usiyeelewa Maandiko, na ni rahisi kudanganywa na kupotea kabisa, maana moyo wako unajaa mapokeo tu. Hujui Neno linasemaje.
Lazima ujue kuwa kila mapokeo lazima yajithibitishe katika msingi wa Neno la Mungu.

Jambo la tatu tunalojifunza katika andiko hilo ni: Kushika lililo jema.
Wakati mwingine unabii unatolewa, lakini kwa namna uwasilishaji ulivyo unaweza kuambatana na mifano au nadharia fulani. Ukizitumia nadharia hizo kama nguzo ya utimilifu wa unabii huo, unaweza kukosa msingi mzuri wa kusimamia.

Sasa Neno linatuambia, "Shika lililo jema." Wewe muombe Mungu akuwezeshe kutambua na kujua lililo jema katika kila jambo.
Pia Mtume Yohana anasema katika 1 Yohana 4:1
"Wapenzi, msiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho kwamba zimetokana na Mungu."

Kwa hiyo Mkristo mwenye hekima hapokei kila unabii kwa sababu tu umetolewa kwa nguvu au kwa ushawishi mkubwa. Kila unabii lazima upimwe kwa Neno la Mungu, kwa tabia ya mtoa unabii, na kwa ushuhuda wa Roho Mtakatifu ndani yako.

Kuna namna, kama uko vizuri na Mungu, utajua tu kuwa huu ujumbe au unabii umetoka kwa Mungu. Na kuna wakati unajua tu kuwa huu ujumbe, pamoja na kutoka kwa Mungu, lakini muwasilishaji kama mwanadamu mwingine kuna kughafilika. Kwa hiyo unapaswa kuchukua lililo jema tu, mengine yaache yapite, maana huo ndio ubinadamu.

Na kuna ujumbe ukiusikiliza unajua kabisa, na Roho Mtakatifu anakushuhudia kabisa, kuwa hapa Mungu hajasema au Mungu hayupo. Na hii ndiyo maana ya kuzijaribu au kuzipima hizo roho kama zimetokana na Mungu.

JE, UNABII UNAOTIMIA NI UPI NA USIOTIMIA NI UPI?

Hapa ndipo katikati ya mjadala wetu wa leo.

Unabii Unaotimia ni Upi?

Unabii unaotimia ni ule unaotoka kwa Mungu na ambao wakati wake wa kutimia umefika, au masharti yake yametimizwa.

Mungu akisema neno lisilo na masharti, lina nguvu ya kutimia kwa wakati wake.

Nabii Habakuki katika kitabu cha Habakuki 2:3 anatukumbusha. Anasema hivi:

"Maana njozi hii bado ni kwa wakati ulioamriwa, inafanya haraka ili kuufikilia mwisho wake, wala haitasema uongo; ijapokawia, ingoje; kwa kuwa haina budi kuja, haitakawia."

Umeona hapo, mwana wa Mungu?
Wakati mwingine unabii haujafa; Ni unasubiri tu wakati wake.

Unabii Usiotimia (Au Unaobatilika) ni Upi?

Hapa ndipo watu wengi wanapochanganyikiwa.

Kuna unabii ambao hauonekani kutimia kwa sababu Mungu ameonyesha rehema zake kutokana na toba au maombi ya mtu. Pia kuna unabii unaoshindwa kutimia kwa sababu haukutoka kwa Mungu tangu mwanzo.

KUBATILIKA KWA UNABII

Bwana Yesu asifiwe sana!

Unabii unaweza kubatilika kwa sababu ya mambo kadhaa.

Hebu tuangalie mifano ya Biblia.

A. Kubatilika kwa Njia ya Toba (Hapa Tutatazama Kisa cha Ninawi)

Tunakubaliana wote kuwa Mungu alimtuma Nabii Yona kwenda Ninawi akiwa na ujumbe wa hukumu usemao:

"Baada ya siku arobaini Ninawi utapinduliwa."

Lakini watu wa Ninawi waliposikia, walitubu mbele za Mungu. Na Mungu alighairi mabaya juu ya Ninawi na watu wake.

Hebu tusome wote Yona 3:10.

Inasema:
"Mungu akaona matendo yao, ya kuwa wameigeuka njia yao mbaya; Mungu akalighairi lile baya, ambalo alisema atawatenda; asilitende."

Sasa nikuulize:
Je, Yona alikuwa nabii wa uongo?
Jibu ni Hapana.
Huu ni mfano wa unabii wa hukumu uliosimamishwa kwa sababu ya toba ya watu.

B. Kubatilika kwa Njia ya Rehema za Mungu (Tuangazie Kisa cha Hezekia)

Mfalme Hezekia aliugua, na Mungu akamtuma Nabii Isaya akiwa na ujumbe huu:

 "Tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona."

Hili tunalisoma katika 2 Wafalme 20:1

Lakini tunasoma mambo yaligeuka baada ya Hezekia alijinyenyekeza mbele za Mungu na kuomba kwa machozi.
Mungu akamjibu kupitia Isaya, kama ilivyoandikwa katika 2 Wafalme 20:5: ikisema
"Nimeyasikia maombi yako, nimeyaona machozi yako; tazama, nitakuponya."
Na hatimaye Mungu alimwongezea miaka kumi na mitano ya kuishi.

Kisa hiki kinatuonyesha kuwa Mungu ni mwingi wa rehema, na kwamba baadhi ya matamko ya hukumu yanaweza kubadilishwa pale mtu anaponyenyekea mbele zake kwa toba na maombi ya dhati.
Lakini hii haimaanishi kuwa kila unabii unaweza kubatilishwa na mwanadamu, bali inaonyesha ukuu wa rehema za Mungu juu ya maisha ya watu wake.

Hata hivyo, mwana wa Mungu, ni muhimu kuelewa kuwa si kila unabii usiotimia huwa ni wa uongo. Baadhi ya unabii wa Mungu huwa na masharti ya utii, toba au majira maalumu ya kutimia.

C. Upande wa Pili: Unabii wa Uongo (Hautatimia Kamwe)
Mwana wa Mungu, hapa ndipo tunapaswa kuwa waangalifu sana.

Biblia inatufundisha kuwa si kila anayesema, "Bwana amesema," kweli ametumwa na Mungu.
Wapo manabii wa uongo ambao hunena kutokana na mawazo yao wenyewe, tamaa zao, au hata roho za udanganyifu.

Mungu anasema katika Yeremia 23:21:
"Sikuwatuma manabii hao, lakini walipiga mbio; sikusema nao, lakini walitabiri."

Pia katika Yeremia 14:14, Mungu anazungumza akisema:
"Manabii wanatabiri uongo kwa jina langu; sikuwatuma, wala sikuwaamuru, wala sikusema nao."


Mfano mwingine ni Hanania katika Yeremia 28. Alitabiri kwamba utumwa wa Babeli ungeisha ndani ya miaka miwili, lakini Mungu alikuwa hajasema hivyo. Mwishowe neno lake halikutimia, na hukumu ya Mungu ikamfikia.

Ndiyo maana Biblia inatoa kipimo hiki katika Kumbukumbu la Torati 18:22:
"Atakaponena nabii kwa jina la BWANA, lisifuate neno lile wala halikutimia, hilo ndilo neno asilolinena BWANA; kwa kujikiai wake amelinena huyo nabii, usimwogope."

Kwa hiyo, kutotimia kwa unabii kunaweza kuwa ishara kuwa neno hilo halikutoka kwa Mungu kabisa.

TAFAKARI YA MWISHO KUTOKA KWANGU

Mwana wa Mungu, kupitia somo hili tumeelewa kuwa suala la unabii linahitaji hekima, utulivu na ufahamu wa Maandiko.

Tumeona kuwa kuna unabii ambao hutimia kwa wakati wake uliowekwa na Mungu. Tumeona pia kuwa yapo matamko ya hukumu ambayo Mungu, kwa rehema zake, anaweza kuyasimamisha pale mtu au taifa linapotubu na kurejea kwake.

Vilevile tumejifunza kuwa si kila neno linalojiita unabii linatoka kwa Mungu. Biblia inatuagiza kupima kila jambo kwa Neno la Mungu, na kutokubali kila sauti inayodai kuzungumza kwa niaba ya Mungu.

Kwa hiyo, mwana wa Mungu, usijenge maisha yako juu ya unabii pekee. Jenga maisha yako juu ya Kristo Yesu na Neno lake. Unabii wa kweli humsogeza mtu karibu na Mungu, humjenga katika imani, na haumwondoi kamwe kwenye msingi wa Maandiko Matakatifu.

Kazi yako si kukimbizana na kila mtu anayetoa unabii, bali ni kudumu katika ushirika na Mungu, kujifunza Neno lake, kuomba, na kupima kila jambo kwa kweli ya neno la Mungu.

Mungu akubariki sana kwa kuwa nami katika makala hii. Ni furaha yangu kukuona ukiwa nami pia katika makala nyingine ninazofuata.

Ubarikiwe sana.

Makala hii imeandaliwa na mimi, mwandishi wako;
Samwel Ombeni.


Je, umejifunza kitu kipya na cha kukujenga kiimani leo?

Kama una swali, maoni, au unahitaji msaada wa ufafanuzi juu ya mada hii ya leo, milango yetu iko wazi. Andika maoni yako hapa chini kwenye blogu yetu ya VICTORY IN CHRIST.

Mungu wa mbinguni akubariki, akulinde, na akupe ushindi katika Kristo Yesu. Amen!

Comments

Popular posts from this blog

JE MUIMBAJI WA PRAISE AND WORSHIP NI NANI?

Je, Ushuhuda Wako Unajenga au Unaua Imani ya Wengine?