Je, Ushuhuda Wako Unajenga au Unaua Imani ya Wengine?


SOMO: Jinsi Shuhuda Zinavyokuza au Kudumaza Imani ya Mkristo?

Bwana Yesu asifiwe sana, mtu wa Mungu. 

Namshukuru sana Mungu kwa kunipa kibali cha kukutana nawe tena, mfuatiliaji wa makala zangu.

Ni neema kubwa kwangu kuwa mshirika wako katika kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu Neno la Mungu na maisha ya Mkristo.

 Leo natamani tuongozane tena tujifunze kuhusu shuhuda.

Bila shaka umewahi kusikia watu wengi, na hasa katika jamii ya Wakristo, wakizungumza kuhusu shuhuda.Wapo wanaoeleza jinsi Mungu alivyowatendea makuu na namna ushuhuda wao ulivyobadili maisha yao na kuimarisha imani yao.

Wengine pia wameeleza jinsi baadhi ya shuhuda walizozisikia zilivyowafanya wawe na hofu au tahadhari katika kufanya mambo fulani.

Leo natamani mimi na wewe tusafiri pamoja katika kujifunza kwa kina kuhusu shuhuda. Tutajaribu kujibu maswali muhimu kama vile:

·         Shuhuda ni nini?

·         Kwa nini tunashuhudia?

·         Kazi ya shuhuda ni ipi?

·         Na kwa nini katika baadhi ya makanisa hutengwa muda maalumu kwa ajili ya ushuhuda?

 Ninaamini kwamba mwisho wa somo hili tutakuwa tumepata uelewa mpana kuhusu nafasi ya shuhuda katika maisha ya Mkristo, pamoja na namna zinavyoweza kujenga au, pale zinapotumiwa vibaya, kudumaza imani za watu wengi.

 Bwana Yesu asifiwe sana.

Awali ya yote, ningependa tuanze kwa kujibu swali hili:

Shuhuda ni nini kwa muktadha wa kawaida?

Shuhuda ni Nini katika Muktadha wa Kawaida?

Shuhuda ni kitendo cha kueleza jambo uliloliona, ulilolisikia, au ulilolipitia wewe mwenyewe ili kuthibitisha ukweli wa tukio fulani, kueleza uzoefu fulani binafsi, au kuwapa wengine uelewa kuhusu mambo fulani.

Kwa hiyo, kwa mtazamo wa kawaida, shuhuda ni kueleza uzoefu binafsi na ukweli wa mambo fulani, kwa lengo la kukuza uelewa wa mambo fulani kwa watu fulani.

Kwa kuwa mimi nilipenda tuzungumzie shuhuda na athari zake kwa imani za watu, basi ni dhahiri kuwa lengo la makala hii ni kuzungumzia shuhuda katika muktadha wa kimaandiko zaidi. Sasa ni wakati sahihi wa kujua shuhuda ni nini kwa mujibu wa maandiko.

Shuhuda ni Nini kwa Mujibu wa Biblia?

Bwana Yesu asifiwe.

Kabla ya kuanza ufafanuzi, naomba tusome pamoja Neno la Mungu katika kitabu cha Ufunuo 12:11:

"Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakuyapenda maisha yao hata kufa."

 Pia unaweza kujifunza zaidi kwa kusoma vifungu hivi:

·         Zaburi 66:16

·         Marko 5:19

·         2 Wakorintho 10:17–18

·         Matendo ya Mitume 1:8

·         1 Petro 2:9

Kutokana na Maandiko hayo, tunaweza kusema kwamba:

Shuhuda kwa mujibu wa Maandiko Matakatifu ni kitendo cha kueleza matendo makuu ambayo Mungu ametenda, ili kudhihirisha ukuu wake, uaminifu wake na uwezo wake wa kutenda mambo yasiyowezekana kwa wanadamu.

Kwa maneno mengine,

Shuhuda ni ushahidi wa kweli unaomtangaza Mungu kwa sababu ya matendo yake makuu, tabia yake, ahadi zake na wokovu alioutoa kupitia Yesu Kristo. 

Kwa hiyo, ushuhuda si simulizi ya jambo lililotokea katika maisha ya mtu, wala si hadithi za mambo ya kawaida ya kila siku. Kwa mtazamo wa kibiblia, ushuhuda unamhusu Mungu na yale aliyoyatenda katika maisha ya watu wake.

Ni muhimu pia kufahamu kwamba namna watu wanavyopokea au kutafsiri shuhuda mara nyingi hutegemea kiwango chao cha ukuaji wa kiroho. Wapo waliokomaa katika imani, wapo wachanga kiroho, na wapo ambao bado hawajapata mafundisho ya kutosha kuhusu namna sahihi ya kumshuhudia Mungu.

Ndiyo maana kupitia makala hii natamani kukusaidia kujitathmini na kujiuliza swali hili:

Je, wewe ni mshuhudiaji anayemshuhudia Mungu kwa usahihi, kwa mujibu wa Maandiko Matakatifu?

Je, kwa Nini Tunashuhudia?

Kila mtu wa Mungu, na hasa jamii ya waliookoka, anapaswa kujua kusudi la kutoa ushuhuda. Kushuhudia si jambo la kufanya kwa sababu tu umepewa nafasi ya kuzungumza madhabahuni, wala si kwa sababu unataka watu wakusikilize au wakufahamu. Vivyo hivyo, si jambo la kufanya kwa mazoea au desturi za kanisa. 

Bwana Yesu asifiwe.

Kwa mujibu wa Maandiko Matakatifu, ushuhuda una kusudi maalumu. Mungu hakuruhusu upitie jambo fulani ili ulifurahie peke yako, bali mara nyingi hulitenda pia liwe sababu ya wengine kumjua, kumwamini na kumtukuza.

Katika sehemu hii tutajifunza baadhi ya sababu za msingi zinazotufanya tumshuhudie Mungu, ili kila mmoja wetu ajitathmini kama kweli ushuhuda anaoutoa unatimizwa na kusudi ambalo Mungu alilikusudia.

 

1. Tunashuhudia ili kuwafanya wasiomjua Mungu wamwamini Kristo.

  Ni muhimu kuelewa kwamba moja ya kusudi kubwa la ushuhuda ni kuwavuta watu kwa Kristo. Mara nyingi Mungu hutenda jambo katika maisha ya mtu mmoja ili kupitia ushuhuda wake, wengine wapate kumwamini Yesu Kristo.

Tusome katika Yohana 4:39:

"Na wengi katika Wasamaria wa mji ule wakamwamini kwa sababu ya neno la yule mwanamke aliyeshuhudia, ya kwamba, Aliniambia mambo yote niliyoyatenda."

Hapa tunaona wazi nguvu iliyo ndani ya ushuhuda. Mwanamke Msamaria hakuhubiri mahubiri marefu, bali alisimulia kwa uaminifu kile Mungu alichomtendea. Matokeo yake, watu wengi walimwamini Kristo na kuziamini kazi zake.

Sasa jiulize swali hili:

Je, Mungu amekutendea jambo ambalo likisimuliwa linaweza kuwavuta wengine kwa Kristo, lakini bado umenyamaza?

Wakati mwingine tunafikiri ushuhuda wetu hauna umuhimu, kumbe Mungu anataka kuutumia kama chombo cha kuwavuta wengine kwake.

Ni muhimu kufahamu kwamba ushuhuda si kwa ajili ya kuonyesha ubora tulio nao, au namna Mungu anavyotupendelea sana, bali ni wa kumfunua Kristo kwa wale ambao bado hawajamjua. 

Kwa hiyo, tunaposhuhudia kwa usahihi tunakuwa tunashiriki katika kazi ya kueneza Injili na kuwafanya watu wengi zaidi wamwamini Bwana Yesu.

2. Tunashuhudia ili Kumtukuza Mungu na Kutangaza Matendo Yake.

Kusudi kubwa la ushuhuda vilevile ni kumtukuza Mungu na kutangaza matendo yake makuu. Ili ushuhuda utimize kusudi hilo, ni lazima ushuhuda  huo umwelekeze msikilizaji kwa Mungu, si kwa mwanadamu.

Kwa kweli, kama wewe ni Mkristo na umeokoka, unapaswa kufahamu kwamba kushuhudia si jambo la hiari tu, bali ni sehemu ya wito wako wa kumtangaza Mungu na matendo yake.

Tusome Neno la Mungu katika 

1 Petro 2:9:

 "Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu." (mwisho wa kunukuu)

 Maandiko haya yanatuonyesha wazi kwamba Mungu ametuita ili kuzitangaza fadhili zake. Hivyo, tunapotoa ushuhuda wa kweli, tunakuwa tunatimiza sehemu ya kusudi ambalo Mungu ametuitia. 

Vilevile, katika Marko 5:19, Yesu alimwambia yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo:

"…….Enenda nyumbani kwako kwa watu wako, ukawaambie jinsi Bwana alivyokutendea makuu, na jinsi alivyo kurehemu."

 Angalia hapa, Yesu hakumwambia aende akajitangaze yeye mwenyewe, wala hakumwagiza awatangazie watu uwezo wake binafsi. Alimwagiza akaeleze mambo makuu aliyotendewa na Bwana.

Hapa ndipo tunajifunza kwamba ushuhuda sahihi humwelekeza msikilizaji kwa Mungu. Unawafanya watu waone ukuu wa Mungu, huruma yake, uaminifu wake na uwezo wake wa kutenda katika maisha ya wanadamu.

Kwa hiyo, kila tunapotoa ushuhuda, ni vizuri tujiulize swali hili:

 Je, ushuhuda wangu unalitukuza jina la Mungu, au unawafanya watu walione zaidi jina langu au la mwanadamu mwingine?

 Kwa sababu lengo la ushuhuda si kumwinua mwanadamu, bali ni kumwinua Mungu aliyefanya jambo hilo. 

3. Tunashuhudia ili Kumtangaza Kristo kwa Watu. 

Bwana Yesu asifiwe.

Sababu nyingine muhimu inayotufanya tumshuhudie Mungu ni kumtangaza Yesu Kristo kwa watu. Hili ndilo kusudi kuu la ushuhuda wa mtu wa Mungu. Tunaposhuhudia, hatupaswi kuwafanya watu wavutiwe nasi, bali wanapaswa kuvutwa kwa Kristo. 

Tusome Neno la Mungu katika Matendo ya Mitume 1:8

"Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi."

Maneno haya yalizungumzwa na Bwana Yesu kabla hajapaa kwenda mbinguni. Aliwaahidi wanafunzi wake kwamba watapokea nguvu za Roho Mtakatifu, na matokeo yake wangekuwa mashahidi wake.

Ni vizuri kujua kwamba Yesu hakusema watakuwa mashahidi wa miujiza, wa makanisa yao, wala wa viongozi wao. Alisema, "mtakuwa mashahidi wangu." Hii inaonyesha kwamba lengo la ushuhuda ni kumtangaza Kristo na kuwafanya watu wamjue yeye.

Pamoja na hayo, tunaona kuwa ushuhuda halisi hauwezi kutenganishwa na kazi ya Roho Mtakatifu. Ni Roho Mtakatifu anayempa Mkristo ujasiri, hekima na uwezo wa kumshuhudia Kristo kwa usahihi.

Kwa hiyo, tunajifunza kwamba ushuhuda si kwa ajili ya kujionyesha, wala si kwa ajili ya kutafuta sifa kutoka kwa watu. Kusudi la ushuhuda ni kumtangaza Kristo, kumthibitisha mbele za watu, na kuwavuta wengi wamwamini yeye..

Ni vizuri kila mmoja wetu ajiulize:

Je, ushuhuda ninaoutoa unawavuta watu kwa Yesu Kristo, au unawafanya wavutiwe zaidi na mimi au mwanadamu mwingine?

Kila ushuhuda unaotolewa unapaswa kumfanya msikilizaji atamani kumjua Kristo zaidi, na kumfuata kwa moyo wote.

 Sababu ingine ya kwanini tunashuhudia ni hii;

 

4. Tunashuhudia ili Kulijenga Kanisa na Kuwaimarisha Washirika (waumini).

Bwana Yesu asifiwe.

Kumshuhudia Mungu ni kulijenga Kanisa na kuwaimarisha waumini katika imani yao.

Tukisoma habaei za mtume Paulo tunaona Kuna wakati Mtume Paulo alitamani sana kulitembelea Kanisa la Rumi. Lengo lake halikuwa kwenda kujionyesha wala kutafuta sifa, bali kuwaimarisha waumini (washirika kwa lugha ya leo) na kufarijiana pamoja katika imani.

Tusome Neno la Mungu katika Warumi 1:11–12:

"Kwa maana natamani sana kuwaona, nipate kuwapa karama ya rohoni, mpate kuthibitishwa; yaani, tufarijiane kwa imani iliyo yenu na iliyo yangu, mimi na ninyi."

Maandiko haya yanatufundisha kwamba katika Kanisa la Kristo, kila mmoja ana wajibu wa kumjenga mwenzake katika Imani. Na wajibu huo ni pamoja na kuelezana kwa njia ya shuhuda kila mmoja na vile Mungu alivyomtendea, alivyomvusha au hata kumuepusha na hatari flani.

Hata hivyo Baadaye, Paulo alifika Rumi akiwa mfungwa. Ingawa alikuwa chini ya ulinzi, hakuliacha kusudi ambalo Mungu alikuwa amempa. Aliendelea kuwafundisha waliokuwa wakimtembelea na aliandika nyaraka nyingi ambazo zimeendelea kulijenga Kanisa kote ulimwenguni hadi leo.

Habari hii tunaisoma vema katika Matendo ya Mitume 28:30–31: 

"Akakaa muda wa miaka miwili mizima katika nyumba aliyojipangia mwenyewe, akiwakaribisha wote waliomwendea, akihubiri ufalme wa Mungu, na kufundisha habari za Bwana Yesu Kristo kwa ujasiri wote, pasipo kuzuiliwa."

 Hili linatufundisha kwamba hata mazingira magumu hayakumzuia Paulo kuendelea kuwajenga watu wa Mungu. Vivyo hivyo, ushuhuda wa kweli unapaswa kuwa chombo cha kulijenga Kanisa, kuwaimarisha waamini na kuwafanya wakue katika kumwamini Kristo.

Kwa hiyo, :

  Ushuhuda unapaswa kulijenga Kanisa la Mungu, na sio kuwaacha watu wakiwa na maswali, mashaka au migawanyiko?

Kila ushuhuda unaotolewa unapaswa kuwa sababu ya waumini wengine kuimarika katika imani, kuongezeka katika upendo wa Kristo na kuzidi kumtumaini Mungu.

5. Tunashuhudia ili Kuwatia Moyo Walio Dhaifu katika Imani.

Sababu nyingine muhimu inayotufanya tumshuhudie Mungu ni kuwatia moyo wale walio dhaifu katika imani.

Ni vizuri kuelewa kwamba si waumini wote wana kiwango kinachofanana cha imani. Wapo ambao wamekomaa katika imani, na wapo ambao bado ni wachanga kiroho. Wengine husimama imara hata wanapopitia majaribu makubwa, lakini wengine hukata tamaa hata wanapokumbana na changamoto ndogo.

Bila shaka wengi wetu tumewahi kuona hali hii. Kuna mtu humwomba Mungu jambo fulani, lakini akiona limechelewa kutokea kwa siku chache au wiki kadhaa, huanza kukata tamaa na hata kuhoji kama Mungu bado anamsikia.

Katika hali kama hiyo, ushuhuda wa kweli unaweza kuwa chanzo cha faraja na kuamsha tumaini jipya. Mtu anaposikia jinsi Mungu alivyomtendea mwingine, anaweza kutiwa moyo kuendelea kumtumaini Mungu na kutokata tamaa.

Ndiyo maana Mtume Paulo aliandika katika 2 Wakorintho 1:3–4:

"Na ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa rehema na Mungu wa faraja yote; atufarijie katika dhiki zetu zote, ili sisi nasi tupate kuwafariji wale walio katika dhiki yo yote, kwa faraja ile ile ambayo sisi wenyewe tunafarijiwa na Mungu."

Maandiko haya yanatufundisha kwamba Mungu hutufariji ili nasi tuweze kuwafariji wengine. Vivyo hivyo, Mungu anatenda mambo katika maisha yetu ili kupitia ushuhuda wetu, wengine wapate nguvu ya kuendelea kusimama katika imani.

Kwa hiyo, ushuhuda wa sahihi haupaswi kuwafanya watu wakate tamaa, bali unapaswa kuwainua, kuwafariji na kuwajengea tumaini kwamba Mungu bado anatenda kazi hata katika maisha yao.

Kumbuka kwamba kusudi la ushuhuda si kuwaonyesha watu jinsi tulivyo wakubwa, bali kuwaonyesha jinsi Mungu alivyo mwaminifu. Na ushuhuda unaomwelekeza mtu kumtumaini Mungu huwa umeitimiza sehemu ya kusudi kuwapo kwa shuhuda.

 

6. Tunashuhudia ili Kuwafundisha Watu Subira na Uvumilivu

Bwana Yesu asifiwe, watu wa Mungu.

Sababu nyingine inayotufanya tumshuhudie Mungu ni kuwafundisha watu subira na uvumilivu wanapopitia majaribu na changamoto mbalimbali za maisha.

Ni kweli kwamba kila mmoja wetu anatamani kuona Mungu akijibu maombi yake kwa haraka. Lakini Neno la Mungu linatufundisha kwamba Mungu ana wakati wake wa kutenda, na mara nyingi hutumia kipindi cha kusubiri kutujenga katika imani, kutufundisha uvumilivu na kutukomaza kiroho.

Hebu tumwangalie Ayubu, mtumishi wa Mungu.

Tukisoma habari za Ayubu tunaona pamoja na kupitia majaribu makubwa, kupoteza mali zake, watoto wake na hata afya yake kudhoofika, Ayubu hakuacha kumtumaini Mungu. Watu waliokuwa karibu naye walidhani kwamba huenda alikuwa amemkosea Mungu, lakini Ayubu aliendelea kusimama katika uaminifu wake.

Je Kama ungekuwa wewe ndiye Ayubu, je, ungeweza kuvumilia majaribu yale bila kumwacha Mungu?

Maandiko yanatuambia katika Yakobo 5:10–11:

"Ndugu zangu, watwaeni manabii walionena kwa jina la Bwana, wawe mfano wa kustahimili mabaya na wa kuvumilia. Angalieni, twawaita heri wale waliostahimili. Mmesikia habari ya ustahimilivu wa Ayubu, mmeuona mwisho wa Bwana, ya kuwa Bwana amejaa huruma, naye ni mwingi wa rehema."

Neno la Mungu hapa linatufundisha kwamba watu waliovumilia katika majaribu waliwekwa kuwa mifano kwa ajili yetu. Mungu aliruhusu maisha yao yaandikwe katika Biblia ili yatufundishe kwamba mwisho wa wale wanaomtumaini Mungu huwa ni mwema.

Ndiyo maana ushuhuda wa mtu aliyedumu katika imani, licha ya kupitia majaribu makubwa, unaweza kuwajenga wengine wasiache kumtumaini Mungu wanapochelewa kuona majibu ya maombi yao.

Ni muhimu kuelewa kwamba wakati mwingine ushuhuda mkubwa si ule unaoeleza jinsi Mungu alivyokutendea kwa haraka, bali ni ule unaoonyesha jinsi Mungu alivyokupa neema ya kuvumilia mpaka wakati wake ulipotimia.

Kwa hiyo, ushuhuda wa kweli unapaswa kuwafundisha watu kwamba subira si ishara ya Mungu kutokuwasikia, bali mara nyingi ni sehemu ya maandalizi yake kwa kile alichowaandalia.

Sijui unawaza nini juu ya somo hili, lakini bado imani yangu ni kwamba kuna jambo unaendelea kujifunza hapa.

Kama ningeweza kukuliza swali ningekuuliza swahili hili 

Je, ushuhuda wako unawafundisha watu kusubiri majira ya Mungu, au unawajengea matarajio kwamba Mungu lazima atende kwa wakati unaotarajiwa na mwanadamu?

 Bila shaka jibu ulilonalo linakupa msukumo chanya wa namna ya kufanya ushuhuda wako uwafaee watu wengi zaidi na vilevile umrudishie Mungu utukufu.

  

7. Tunashuhudia Kuzifunua Hila za Adui

Bwana Yesu asifiwe sana.

Sababu nyingine inayotufanya tumshuhudie Mungu ni kuzifunua hila za adui, ili watu wapate maarifa na wawe waangalifu dhidi ya mbinu ambazo Shetani huzitumia kuwaharibu.

Ni kweli kwamba lengo kuu la ushuhuda ni kumtukuza Mungu. Hata hivyo, wakati mwingine Mungu huruhusu mtu apitie mapito fulani ili baadaye ushuhuda wake uwe fundisho kwa watu wengine. Kupitia ushuhuda huo, wengi hujifunza namna ambavyo Shetani hufanya kazi, huku wakizidi kumtumaini Mungu aliyewaokoa.

Kwa mfano, kuna watu ambao Mungu amewatoa katika vifungo vya ushirikina, uchawi, ibada za sanamu na aina nyingine za utumwa wa kiroho. Wengine wamepitia mateso makubwa kwa sababu ya hila za adui, lakini Mungu akawaokoa. Wanapotoa ushuhuda wao kwa unyenyekevu na kwa hekima, huwasaidia watu kutambua mbinu za adui na kuwa waangalifu zaidi.

Mtume Paulo aliandika katika kitabu cha 2 Wakorintho 2:11:

"............. Shetani asipate kutushinda; kwa maana hatukosi kuzijua fikira zake."

Maandiko haya yanatuonyesha kwamba Mungu hataki watu wake wakose maarifa kuhusu hila za Shetani. Kuzitambua hila hizo si kwa ajili ya kuutukuza ufalme wa giza, bali ni kwa ajili ya kujifunza namna ya kusimama imara katika Mungu.

Vilevile, Isaya 42:22 inasema:

"Lakini watu hawa ni watu walioibiwa na kutekwa; wote wamenaswa katika mashimo, wamefichwa katika magereza; wamekuwa mateka, wala hapana aokoaye; wamekuwa nyara, wala hapana asemaye, Rudisha."

Andiko hili linatuonyesha kuwa kutekwa ni jambo ambalo linaweza kumpata mwanadamu kwa sababu ibilisi aliye baba wa uongo hutumia hila kuwapotosha wanadamu na hata wakati mwingine kuwatumikisha. Lakini tunaposhuhudia matendo ya Mungu ya ukombozi, tunawatia moyo watu wajue kwamba hakuna kifungo ambacho Mungu hawezi kukivunja, na hakuna mtego wa adui ambao Kristo hawezi kuushinda.

Hata hivyo, ni muhimu sana kuhakikisha kwamba tunapotoa ushuhuda wa aina hii, hatuujengi ufalme wa giza katika fikra za watu, bali tunamtukuza Kristo aliyeshinda nguvu zote za adui. Kusudi la ushuhuda si kuwafanya watu wamuogope Shetani na ufalme wa giza, bali ni kuwafanya wamtumaini Yesu Kristo zaidi na kumhimidi yeye huku wakijua adui naye yu kazini akitafuta kuwashinda na kuwaangusha.

Kwa hiyo, kila ushuhuda unaohusu hila za adui unapaswa kumalizika kwa kumwinua Yesu Kristo, kwa sababu ushindi si wa Shetani, bali ni wa Bwana wetu Yesu Kristo.

 

8. Tunashuhudia ili Kumdhoofisha Shetani na Kuudhihirisha Ushindi wa Kristo

Bwana Yesu asifiwe!

Sababu nyingine inayotufanya tumshuhudie Mungu ni kwamba, kupitia ushuhuda wa kweli, ufalme wa Shetani hudhoofishwa na ushindi wa Yesu Kristo huonekana wazi.

Ni muhimu kuelewa kwamba Shetani hafurahii hata kidogo watu wanapomjua Mungu na kuendelea kukua katika imani. Ndiyo maana hutafuta kila njia ya kuwazuia watu wasimjue Kristo au kuwarudisha nyuma wale ambao tayari wameanza safari ya wokovu.

Lakini Mungu anapotenda jambo kubwa katika maisha ya mtu, na mtu huyo akasimama hadharani kulishuhudia, ushuhuda huo huwafanya watu wengi wamjue Kristo, wamtumaini na waamini kwamba Mungu bado anatenda kazi hata katika kizazi cha sasa.

Kwa namna hiyo, ufalme wa Mungu huendelea kujengwa, na kadiri ufalme wa Mungu unavyojengwa ndani ya mioyo ya watu, ndivyo nguvu za Shetani zinavyozidi kupoteza nafasi yake.

Biblia inasema katika Ufunuo 12:11:

    "Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakuyapenda maisha yao hata kufa."

Andiko hili linatuonyesha kwamba ushindi haukutokana na ushuhuda peke yake, bali ulianza kwa damu ya Mwana-Kondoo, yaani kazi ya Yesu Kristo msalabani. 

Hata hivyo, ushuhuda wao ulikuwa sehemu ya kudhihirisha ushindi huo. Hawakunyamaza,bali waliendelea kumkiri Kristo hata walipokabiliwa na mateso na hatari ya kufa.

Hii inatufundisha kwamba ushuhuda wa kweli una nguvu kwa sababu humtangaza Kristo aliyeshinda. Kadiri watu wanavyozidi kumjua Kristo kupitia ushuhuda, ndivyo hila za Shetani zinavyoendelea kushindwa katika maisha yao.

Ni muhimu pia kufahamu kwamba hatumdhoofishi Shetani kwa uwezo wetu, bali kwa ushindi ambao Yesu Kristo tayari ameupata. Sisi tunakuwa mashahidi wa ushindi huo kwa kuutangaza na hapa pale anapojidhihirisha kwetu.

Kwa hiyo, kila ushuhuda unaotolewa kwa lengo la kumtukuza Mungu huwa unachangia kuwavuta watu kutoka katika ufalme wa giza na kuwaelekeza katika ufalme wa nuru wa Kristo.

Baada ya kujifunza sababu mbalimbali zinazotufanya tumshuhudie Mungu, sasa ni wakati wa kuangalia upande mwingine wa somo hili.

Kwa sababu, pamoja na kuwa shuhuda zinaweza kujenga imani za watu, zikitumiwa vibaya zinaweza pia kudumaza imani za watu wengi.

Hivyo basi, hebu sasa tuanze kujifunza:

Jinsi Matumizi Mabaya ya Shuhuda Yanavyoweza Kudumaza Imani za watu wengi.

Bwana Yesu asifiwe.

Katika sehemu hii napenda tushirikishane mambo kadhaa yatakayotupa msingi mzuri wa kumtumikia Mungu, hasa katika suala la kutoa shuhuda.

Wakati mwingine tunakosea, lakini tunashindwa kuambiwa ukweli kwa sababu ya namna tulivyojijengea mazingira ya kutokukubali kukosolewa. Wengine huogopwa kwa sababu ya nafasi walizonazo, wengine kwa sababu ya ukali wao, na wengine kwa sababu wanaona kila anayewarekebisha ni adui yao.

Lakini mimi leo kwa upendo na unyenyekevu, natamani nikushirikishe jambo moja muhimu. Kama wewe ni mtu mwenye nia ya kweli ya kumpendeza Mungu, basi ni lazima ukubali kufundishwa, kuonywa na kurekebishwa pale inapobidi.

Hakuna mwanadamu mkamilifu mbele za Mungu. Sote tunajifunza kila siku, na ndiyo maana Mungu ameweka vipawa mbalimbali ndani ya Kanisa ili tujengane, tushauriane na kusaidiana kukua katika kweli.

Bwana Yesu asifiwe!

Hebu jiulize swali hili:

Unaweza kuwa unampendeza Mungu katika maeneo mengi ya maisha yako, lakini je, ikiwa hukubali kurekebishwa, hali hiyo haitakuwa kikwazo katika ukuaji wako wa kiroho?

Mimi naamini haipendezi.

Bwana Yesu asifiwe sana.

Siku moja nilisikia kuhusu utaratibu wa dhehebu fulani ambapo watu walikuwa wakitoa shuhuda madhabahuni kwa kumsifu kiongozi wao kupita kiasi. Badala ya kueleza yale Mungu aliyowatendea, walielekeza sifa zote kwa mwanadamu, wakidai kwamba ndiye aliyewatendea mambo makuu. Wengine walifika hata hatua ya kupiga magoti mbele yake au kuanguka miguuni pake kana kwamba walikuwa wakifanya hivyo kwa Mungu. Wengine walienda mbali wakawa wanaimba na nyimbo za kumsifu kama Mungu asifiwavyo

Niliposikia jambo hilo nilibaki nikitafakari sana.

Nikajiuliza, je, lengo halisi la ushuhuda ni kumtukuza Mungu au kumwinua mwanadamu?

Ndipo nikagundua jambo moja muhimu. Mara nyingi Shetani anapotaka kumpotosha mtu, huanza kwa kuharibu ufahamu wake. Mtu anapopoteza ufahamu wa kweli ya Neno la Mungu, huwa vigumu kutambua lililo sahihi na lililo potofu.

Ndiyo maana leo natamani tushirikiane kujifunza jinsi matumizi mabaya ya shuhuda yanavyoweza kudumaza imani za watu taratibu, mpaka mtu akabaki na mapokeo ya dini bila kuwa na msingi imara wa Neno la Mungu. Na mtu asiye na msingi imara wa Neno la Mungu ni rahisi kutikisika na kila upepo wa mafundisho uvumao.

Kwa hiyo, hebu sasa tuangalie baadhi ya aina za shuhuda ambazo, badala ya kuwajenga watu katika imani, zinaweza kuanza kudhoofisha imani zao bila wao wenyewe kutambua.

Zifuatazo ni baadhi ya aina ya shuhuda zinazoweza kudumaza imani za watu.

 

(i) Shuhuda Zinazowasifu na Kuwatukuza Wanadamu Kuliko Yesu Kristo

Bwana Yesu asifiwe sana.

Kuna watu ambao Mungu amewatendea mambo makubwa sana, na kwa kweli wanakuwa na ushuhuda mzuri wa kumtukuza Mungu. Hata hivyo, namna wanavyoutoa ushuhuda huo wakati mwingine huacha picha kwamba mtu aliyewasaidia au aliyekuwa karibu nao ndiye chanzo cha muujiza ule.

Ni kweli kabisa kwamba tunapaswa kuwaheshimu watumishi wa Mungu. Vilevile, si vibaya kumshukuru mchungaji, askofu au mtumishi wa Mungu ambaye amekuwa msaada katika maisha yako ya kiroho. Mimi binafsi sioni tatizo katika hilo.

Lakini kuna jambo moja ambalo tunapaswa kuliangalia kwa makini.

Ikiwa mtu anayetoa ushuhuda hajui kusudi halisi la ushuhuda, ni rahisi sana kuvuka mpaka na kujikuta anamwinua mwanadamu kuliko Mungu aliyefanya jambo hilo.

Bila shaka tunakubaliana kwamba kusudi la ushuhuda ni kumtukuza Mungu kwa yale aliyoyatenda. Vilevile, ushuhuda unapaswa kuwajenga watu katika kumtumaini Mungu, kuwaimarisha walio dhaifu katika imani na kuwafanya wengi wajue kwamba Mungu bado anatenda kazi hata leo.

Sasa swali la kujiuliza.

  • Je, ushuhuda wako unawafanya watu wamjue Mungu zaidi, au unawafanya walijue zaidi jina la mtumishi wako?  au
  • Je, baada ya watu kusikia ushuhuda wako wanatamani kumtafuta Yesu Kristo, au wanatamani kumtafuta yule mtu uliyekuwa ukimsifia?

Bwana Yesu asifiwe sana.

Ni muhimu sana kuelewa kwamba wakati mwingine tunaweza kudhani tunamtukuza Mungu, kumbe namna tunavyosimulia ushuhuda wetu inawafanya watu waone kana kwamba utukufu wote unamhusu mwanadamu.

Biblia inasema katika 2 Wakorintho 10:17–18:

"Lakini yeye ajisifuye, na ajisifu katika Bwana. Maana si yeye ajisifuye mwenyewe aliyekubaliwa, bali yeye anayesifiwa na Bwana."

Mtume Paulo anatufundisha kwamba sifa zote zinapaswa kuelekezwa kwa Mungu. Mwanadamu hapaswi kujitwalia utukufu ambao unamhusu Mungu.

Vilevile, tunasoma katika 1 Wakorintho 15:33:

"Msidanganyike; Mazungumzo mabaya huharibu tabia njema."

Huenda ukajiuliza, andiko hili lina uhusiano gani na ushuhuda?

Jambo la kujifunza hapa ni kwamba kila neno tunalolisema hujenga jambo fulani katika fikra za wanaotusikiliza. Kama ushuhuda wetu umejengwa katika kumwinua mwanadamu kuliko Kristo, basi polepole tutakuwa tunawajenga watu kumtegemea mwanadamu badala ya kumtumaini Mungu.

Na jambo hilo likiendelea kwa muda mrefu, linaweza kudhoofisha imani za watu bila wao wenyewe kutambua.

Kwa hiyo, kila tunapotoa ushuhuda, ni vizuri tujiulize swali hili:

Je, baada ya watu kunisikia, watamkumbuka zaidi Yesu Kristo au watamkumbuka zaidi mwanadamu?

Kama ushuhuda wetu haumwinui Kristo, basi kuna uwezekano kwamba umepoteza kusudi lake kuu.

 

(ii) Shuhuda Zinazowajengea Watu Fikra za Kumpangia Mungu Muda wa Kutenda

Bwana Yesu asifiwe.

Inawezekana ukakisoma kichwa hiki ukajiuliza, "Inawezekanaje ushuhuda ukawajengea watu fikra za kumpangia Mungu muda wa kutenda?"

Naomba uelewe jambo moja muhimu. Kila ushuhuda unaotolewa hubeba ujumbe fulani. Vivyo hivyo, kila ushuhuda huacha fundisho fulani katika mawazo ya watu wanaousikia. Ndiyo maana kila mtu anayesimama kutoa ushuhuda anapaswa kujiuliza swali hili:

Je, ushuhuda wangu unawajengea watu fikra zipi?

Kama ushuhuda wako hauwajengi watu kumtumaini Mungu, bali unawajengea fikra kwamba Mungu lazima atende ndani ya muda fulani, basi bila kujua unaweza kuwa umeacha mbegu ambayo baadaye itadhoofisha imani za watu wengi.

Kwa mfano, mtu anaweza kusimama na kusema:

"Nilimwambia Mungu kwamba mpaka saa nane mchana awe amenijibu. Nikatoa sadaka, nikaomba kwa imani, na kweli kabla ya saa nane Mungu alinijibu."

Bila shaka, Mungu anaweza kutenda jambo kama hilo. Hakuna jambo lisilowezekana kwake. Lakini tatizo halipo katika Mungu kutenda kwa wakati huo. Tatizo linaweza kuwa katika namna ushuhuda ulivyowasilishwa.

Kama hautawaeleza watu kwamba Mungu alitenda kwa neema yake, kwa mapenzi yake na kwa wakati aliouona unafaa, unaweza kuwa umejenga ndani yao fikra kwamba kila mtu anaweza kumpangia Mungu muda wa kutenda. 

Matokeo yake, wengi wakifanya hivyo na wasione majibu ndani ya muda waliouweka, huanza kuvunjika moyo, kujiuliza kama Mungu amewakataa, au hata kuona kana kwamba hawana imani ya kutosha au wanaweza kuwaza Mungu ni waupendeleo maana wao hawakujibiwa sawa na walivyoomba.

Lakini Maandiko hayatufundishi hivyo.

Biblia inasema katika Mhubiri 3:1:

"Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu."

Maandiko haya yanatuonyesha kwamba Mungu ana majira yake ya kutenda. Anaweza kuwajibu watu wawili wanaomwomba jambo lilelile, lakini akamjibu mmoja leo na mwingine baada ya miezi kadhaa au hata miaka. Hilo halimaanishi kwamba mmoja anampenda kuliko mwingine. Linaonyesha tu kwamba Mungu hutenda kwa hekima yake na kwa wakati wake mkamilifu.

Hebu tumwangalie pia Lazaro.

Lazaro alipougua, Martha na Mariamu walituma ujumbe kwa Bwana Yesu mapema wakimjulisha hali ya ndugu yao. Kwa mtazamo wa kibinadamu, walitegemea Yesu afike haraka ili amponye.

Lakini jambo la kushangaza ni kwamba Yesu hakwenda mara moja. Alikaa siku mbili zaidi mahali alipokuwa, ndipo baadaye akaenda Bethania.

Yesu alipofika Lazaro alikuwa tayari amekufa na amekaa kaburini siku nne.

Kwa mtazamo wa Martha na Mariamu, Yesu alikuwa amechelewa.

Ndiyo maana Martha alimwambia Yesu katika Yohana 11:21:

"Bwana, kama ungekuwapo hapa, ndugu yangu hangalikufa."

Lakini kwa mtazamo wa Mungu, Yesu hakuwa amechelewa hata kidogo. Alikuwa anatenda kwa wakati uliokuwa utafunua utukufu wa Mungu kwa kiwango kikubwa zaidi.

Baadaye Yesu alimfufua Lazaro kutoka kwa wafu, na watu wengi wakamwamini kwa sababu ya muujiza huo.

Somo kubwa tunalojifunza hapa ni kwamba Mungu hatendi kwa ratiba zetu, bali kwa mapenzi na hekima yake.

Kwa hiyo, tunapotoa ushuhuda ni muhimu sana kutumia hekima ili tusiwajengee watu fikra kwamba Mungu lazima atende kwa muda tunaoutaka sisi.

Badala yake, ushuhuda wetu unapaswa kuwafundisha watu kumtumaini Mungu hata pale majibu yanapoonekana kuchelewa. Kwa sababu Mungu hachelewi; hutenda kwa wakati wake mkamilifu.

 

 (iii). Shuhuda Zinazowafanya Watu Kujijenga katika Kutafuta Ishara na Miujiza Kuliko Kumtafuta Mungu

Bwana Yesu asifiwe sana.

Tatizo lingine kubwa linaloweza kujitokeza kupitia matumizi mabaya ya shuhuda ni pale zinapowajenga watu kutafuta ishara na miujiza kuliko kumtafuta Mungu mwenyewe.

Ni kweli kwamba Mungu ni Mungu wa ishara, maajabu na miujiza. Popote Mungu anapotenda kazi, mara nyingi hujidhihirisha kwa namna mbalimbali. Kwa hiyo, hatuwezi kupinga ukweli kwamba Mungu bado anatenda ishara na miujiza hata leo.

Lakini pamoja na ukweli huo, kuna jambo moja muhimu sana tunapaswa kulifahamu. Tatizo si kuwepo kwa ishara na miujiza; tatizo ni pale watu wanapoanza kuzipenda ishara kuliko kumpenda Mungu anayezifanya.

Naomba tufungue katika Yohana 6:26-27,

 Bwana Yesu anasema:

"Amin, amin, nawaambia, mnanitafuta, si kwa sababu mliona ishara, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba. Kitendeni kazi si chakula chenye kuharibika, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele..."

Bwana Yesu asifiwe.

Maneno haya yanatufundisha jambo kubwa sana. Watu wengi waliokuwa wakimfuata Yesu hawakuwa wanamtafuta kwa sababu walitamani kumjua zaidi au kusikia mafundisho yake. Walikuwa wanamfuata kwa sababu waliona miujiza na walitaka kuendelea kunufaika nayo.

Kwa maneno mengine, walikuwa wanaitafuta karama kuliko Mwenye Karama, walikuwa wanatafuta muujiza kuliko Mwokozi, na walikuwa wanapenda kile Mungu anachoweza kuwapa kuliko Mungu mwenyewe.

Na hali hiyo ndiyo inaweza kujengwa na baadhi ya shuhuda zisipotolewa kwa hekima.

Kwa mfano, mtu anaweza kutoa ushuhuda wake kwa namna ambayo muda wote anaeleza tu ukubwa wa muujiza alioupata, lakini hasemi jinsi tukio hilo lilivyomfanya avutwe zaidi kwa Mungu, lilivyobadilisha maisha yake, au lilivyoongeza uhusiano wake na Kristo.

Matokeo yake, watu wanaousikia ushuhuda huo hujifunza kwamba lengo la kumtafuta Mungu ni kupata miujiza. Wengine huanza kutangatanga kutoka sehemu moja kwenda nyingine wakitafuta mahali penye ishara nyingi zaidi, badala ya kujijenga katika kumjua Mungu kupitia Neno lake.

Lakini Biblia inatufundisha tofauti.

Katika Yeremia 9:23-24 imeandikwa:

"Bwana asema hivi; Mwenye hekima asijisifie hekima yake, wala mwenye nguvu asijisifie nguvu zake, wala tajiri asijisifie utajiri wake; bali ajisifuye na ajisifu kwa sababu hii, ya kwamba ananifahamu mimi na kunijua..."

Maandiko haya yanatuonyesha kwamba jambo la msingi si kupata vitu kutoka kwa Mungu, bali kumjua Mungu mwenyewe.

Vilevile, Bwana Yesu alisema katika Mathayo 12:39:

".....Kizazi kibaya na cha zinaa hutafuta ishara..."

Hapa Yesu hakuwa anakataza miujiza, bali alikuwa anakemea moyo unaotafuta ishara kila wakati huku ukikosa shauku ya kumjua Mungu.

Kwa hiyo, tunapotoa ushuhuda ni muhimu kuhakikisha kwamba tunawaelekeza watu kwa Kristo, si kwa miujiza pekee.

Ni vizuri watu wajifunze kwamba miujiza ni matokeo ya uwepo wa Mungu, lakini kumjua Mungu ndiyo lengo kuu la maisha ya Mkristo.

Kwa kifupi, mtu anayejengwa katika kutafuta ishara kuliko kumtafuta Mungu mara nyingi huonekana kwa mambo kama haya:

  • Husikiliza shuhuda ili ajue njia ya kupata muujiza, si ili amjue Mungu zaidi.
  • Humtafuta Mungu kwa sababu ya kile anachotaka kupokea, si kwa sababu anatamani kuwa na uhusiano naye.
  • Imani yake hutikisika haraka asipoona ishara au muujiza anaoutarajia.
  • Huwa tayari kuhama kutoka sehemu moja kwenda nyingine akifuata miujiza, bila kujali kama mafundisho anayoyasikia yana msingi wa Neno la Mungu.

(iv) Shuhuda Zinazowajengea Watu Fikra za Kujilinganisha na Wengine Badala ya Kumtumaini Mungu.

    Mungu hana njia moja ya kutenda kwa kila mtu. Ingawa ni Mungu yuleyule, namna anavyotenda kazi katika maisha ya watu inaweza kutofautiana kulingana na mapenzi yake, makusudi yake na wakati wake.

Lakini wakati mwingine shuhuda zinapotolewa bila hekima, zinaweza kuwajengea watu fikra za kujilinganisha na wengine badala ya kumtumaini Mungu.

Kwa mfano, mtu anaweza kutoa ushuhuda wa jinsi Mungu alivyomjibu maombi ndani ya muda mfupi, au jinsi alivyompandisha cheo, alivyombariki kifedha, au alivyomponya ugonjwa fulani. Bila kukusudia, ushuhuda huo unaweza kuwaacha baadhi ya watu wakijiuliza:

"Mbona mimi nimekuwa nikimwomba Mungu kwa muda mrefu lakini bado sijapata majibu kama haya?"

Wengine wanaweza kuanza kufikiri:

  • "Labda Mungu hanipendi."

                        Au,

  • "Pengine mimi sina imani kama wengine."

Mawazo ya namna hii yakikua ndani ya mtu, yanaweza kumfanya aanze kukata tamaa na hata kuona kana kwamba Mungu ana upendeleo.

Lakini Maandiko yanatufundisha tofauti kabisa ya kwamba yeye hana upendeleo.

Hebu fungua nami katika Matendo 10:34-35:

Mimi nitasoma mstari mmoja Biblia inasema

"Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo; bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye."

Kwa hiyo, tofauti ya ushuhuda wa mtu mmoja na mwingine haimaanishi kwamba Mungu anampenda mmoja kuliko mwingine. Mungu hutenda kwa hekima yake na kwa kusudi lake katika maisha ya kila mtu.

Jambo hili tunaliona pia katika maisha ya wanafunzi wa Bwana Yesu. Baada ya kufufuka kwake, Petro alipomwona Yohana akimfuata Yesu, akamuuliza:

"Bwana, na huyu je?" (Yohana 21:21).

Lakini Yesu akamjibu:

"Kama nikitaka huyu akae hata nitakapokuja, yakupasa nini? Wewe unifuate mimi." (Yohana 21:22).

Maneno haya yanatufundisha kwamba Mungu ana mpango wa kipekee kwa kila mtu. Petro hakutakiwa kupima maisha yake kwa kuangalia yale ambayo Mungu alikuwa amempangia Yohana. Wito wake ulikuwa ni kumfuata Kristo kwa uaminifu.

Ndivyo ilivyo hata leo.

Tunapotoa shuhuda, ni muhimu kutumia hekima ili tusiwajengee watu fikra za kujilinganisha na wengine. Badala yake, shuhuda zetu zinapaswa kuwafundisha kwamba Mungu ana njia yake ya kufanya kazi katika maisha ya kila mmoja, na kwamba kila mtu anapaswa kuendelea kumtumaini Mungu bila kujipima kwa ushuhuda wa mwingine.

Kwa sababu mtu anapoacha kumtazama Mungu na kuanza kuwatazama wengine, mara nyingi huzaliwa; 

  • wivu, 
  • kukata tamaa, 
  • mashindano yasiyo ya kiroho, 
  • Na hata malalamiko na manung`uniko dhidi ya Mungu.
Jambo jingine linaloweza kuleta uharibifu kama shuhuda hazitatolewa kwa uangalifu ni;

 

(v) Shuhuda Zisizo za Kweli (Shuhuda za Kubuni na za Uongo)

Shuhuda ni ushahidi wa matendo ya Mungu. Kwa hiyo, ili ushuhuda uwe na nguvu mbele za Mungu na mbele za watu, ni lazima uwe wa kweli.

Lakini wakati mwingine watu hutoa shuhuda ambazo si za kweli. Wengine huongeza mambo ambayo hayakutokea, wengine hupunguza ukweli, na wengine hutunga kabisa ushuhuda kwa sababu mbalimbali. 

Wapo wanaotafuta sifa kutoka kwa watu, wengine wanataka waonekane wana imani kubwa, na wengine hufanya hivyo ili wapate kukubalika katika jamii au kusanyiko lao.

Naomba ujiulize swali hili:

Je, Mungu anaweza kutukuzwa kupitia uongo?

Jibu ni hapana.

Biblia inasema katika Mithali 12:22:

"Midomo ya uongo ni chukizo kwa Bwana; Bali watendao uaminifu ndio furaha yake."

Maandiko haya yanatuonyesha wazi kwamba Mungu hufurahishwa na ukweli, lakini huchukizwa na uongo. Kwa hiyo, hata kama mtu anadai anamshuhudia Mungu, ikiwa ushuhuda wake umejengwa juu ya uongo, hauwezi kuwa na kibali cha Mungu.

Vilevile, Mithali 13:5 inasema:

"Mwenye haki huchukia uongo; Bali mtu mbaya hujiletea aibu na fedheha."

Ni muhimu kuelewa kwamba kila ushuhuda hubeba ushawishi fulani kwa watu wanaousikia. Sasa kama ushuhuda huo si wa kweli, je, unawajenga watu katika imani au unawajenga katika udanganyifu?

Hebu fikiria mfano huu.

Mtu anasimama mbele ya watu na kusema:

"Namshukuru Mungu kwa sababu nimeponywa kabisa ugonjwa huu, sasa sina tatizo tena."

Lakini baada ya muda mfupi, watu wanaona bado anaumwa ugonjwa uleule na hata anaendelea na matibabu.

Katika hali kama hiyo, tatizo linaweza kuwa si kwamba Mungu hajatenda, bali ni kwamba ushuhuda ulitolewa kwa haraka au kwa namna isiyo sahihi.

Pengine ingekuwa bora mtu huyo angesema:

"Namshukuru Mungu kwa sababu nimeanza kuona mabadiliko ndani yangu au kwenye mwili wangu."

Kauli ya namna hiyo inaonyesha imani bila kuacha nafasi ya watu kufikiri kwamba Mungu ameshindwa au kwamba ushuhuda ulikuwa wa uongo.

Ni muhimu kukumbuka kwamba Shetani ni baba wa uongo (Yohana 8:44). Kwa hiyo, kila uongo unaoingia katika ushuhuda unaharibu kusudi la ushuhuda wenyewe, ambalo ni kumtukuza Mungu aliye wa kweli.

Nivizuri, tunapotoa ushuhuda tusitafute kuwavutia watu kwa maneno makubwa, bali tuseme ukweli kwa unyenyekevu. Kwa sababu ukweli una nguvu ya kujenga imani, lakini uongo una nguvu ya kubomoa imani.

(vi) Shuhuda Zinazowajengea Watu Imani kwa Mwanadamu Badala ya Neno la Mungu.

Msingi wa imani ya Mtu anayemuamini Mungu haupaswi kuwa uzoefu wa mwanadamu, bali hujengwa katika Neno la Mungu. 

Shuhuda zina nafasi kubwa katika kuwajenga watu, lakini hazikukusudiwa kuchukua nafasi ya Maandiko Matakatifu. Badala yake, zinapaswa kulithibitisha Neno la Mungu na kuwaelekeza watu kwa Kristo.

Tatizo la watu wengi wanajenga imani yao juu ya shuhuda za wanadamu kuliko juu ya Neno la Mungu. Wakati mwingine mtu anaweza kutoa ushuhuda kwa namna ambayo watu wanaishia kuamini kwamba mafanikio yao, uponyaji wao au ukombozi wao unategemea (mhubiri,askofu,mchungaji, nk) badala ya kumtumaini Yesu Kristo.

Ni kweli Mungu huwatumia watumishi wake kutenda kazi zake. Lakini ni muhimu kukumbuka kwamba watumishi wote ni vyombo tu mikononi mwa Mungu.

Hawapaswi kuwa msingi wa imani ya watu, Bali wanaweza kuwa viongozi katka imani au wanaweza kuwa waangalizi wa watu katika mambo ya imani na hii ni kwa sababu hata wao wanamhitaji Mungu kila siku. Utukufu wote wa kazi ya Mungu kwa yale Mungu anayotutendea unapaswa kurudi kwa Mungu peke yake.

Mtume Paulo aliandika katika 1 Wakorintho 3:5-7:

"Basi Apolo ni nani? Na Paulo ni nani? Ni watumishi tu ambao kwao mliamini; tena kila mmoja kama Bwana alivyomjalia. Mimi nilipanda, Apolo akatia maji; bali Mungu ndiye aliyekuwa akikuza. Hivyo, apandaye si kitu, wala atiaye maji, bali Mungu akuzaye."

Maneno haya yanatuonyesha wazi kwamba hata watumishi wakubwa wa Mungu hawakuwataka watu wajenge imani yao juu yao. Walijitahidi kuwaelekeza watu kwa Mungu, kwa sababu walitambua kwamba yeye ndiye chanzo cha uzima, ukuaji na wokovu.

Vilevile, Biblia inasema katika Warumi 10:17:

"Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo."

Imani ya kweli huzaliwa na kukua kwa kulisikia na kuliamini Neno la Mungu. Shuhuda zinaweza kuwatia watu moyo, lakini haziwezi kuchukua nafasi ya Neno la Mungu. Shuhuda ni daraja linalopaswa kuwaongoza watu kwa Kristo; Si mwisho wa safari yao ya imani, bali ni mwazo wa kuongeza imani ya mtu kwa Mungu.

Kwa hiyo, kila tunapotoa ushuhuda ni lazima tuhakikishe kwamba tunawaelekeza watu kwa Yesu Kristo na kwa Neno lake. Tusipofanya hivyo, tunaweza kuwafanya wajenge imani yao juu ya wanadamu, jambo ambalo si kusudi la Mungu.

Kwa kifupi, thamani ya ushuhuda haipimwi kwa ukubwa wa muujiza uliotokea, bali kwa matunda unaoyaacha katika maisha ya watu. Kama baada ya kusikia ushuhuda wako watu wanamkaribia Kristo, wanalipenda zaidi Neno la Mungu na wanazidi kumtumaini yeye, basi ushuhuda huo umetimiza kusudi lake. Lakini kama unawaacha wakimtegemea mwanadamu kuliko Mungu, basi ushuhuda huo unahitaji kutazamwa upya na kumulikwa kwa nuru ile na mwangaza wa Neno la Mungu. 

 

HITIMISHO:

Bwana Yesu asifiwe sana.

Baada ya kutafakari kwa pamoja somo hili, ninaamini sasa tunaweza kuelewa kwamba shuhuda ni zawadi nzuri ambayo Mungu ameipa Kanisa lake kwa kusudi la kumtukuza yeye, kuwaleta watu kwa Kristo, kulijenga Kanisa na kuwafanya watu wakue katika imani. 

Lakini pamoja na uzuri wake, tumeona pia kwamba shuhuda zisipotolewa kwa hekima na kwa kuongozwa na Neno la Mungu zinaweza kuacha mbegu ambazo baadaye hudhoofisha imani za watu badala ya kuzijenga. 

Pengine hapa unaweza ukajiuliza, "Kwa nini Samwel ameona ni muhimu kuandika makala hii?"

Jibu ni rahisi sana.

Kwa sababu nimegundua kwamba watu wengi wanajua umuhimu wa kushuhudia, lakini si wengi wanaojiuliza kama namna wanavyoshuhudia ndiyo ambayo Mungu anataka. Mara nyingi tunafikiri jambo muhimu ni kusimama na kueleza kile Mungu alichotutendea, lakini hatuhoji matokeo ambayo vinywa vyetu vinayaacha katika mioyo ya watu wanaotusikiliza. 

Ndugu yangu, jambo moja ni lazima ulielewe. Mungu anajua alichokutendea. Lakini sisi wanadamu tunamjua Mungu kupitia kile unachotuambia. Ndiyo maana ni muhimu sana kujifunza namna ya kushuhudia kwa hekima, ili kile tunachokisema kisiwajengee watu mitazamo itakayodhoofisha imani zao, bali kiwasaidie kumjua Kristo zaidi na kuliamini Neno lake. 

Ndiyo sababu nimeona ni vema tushirikiane kujifunza somo hili. Si kwa lengo la kuwahukumu wanaoshuhudia, bali ili sisi sote tujifunze namna ya kutumia shuhuda zetu kwa usahihi, kwa utukufu wa Mungu na kwa faida ya watu wake.

Kumbuka, kila neno tunalolisema mbele za watu hubeba mbegu ndani yake. Mbegu hiyo inaweza kujenga imani au kuibomoa. Hivyo basi, na tushuhudie kwa hekima, kwa kweli na kwa unyenyekevu, ili katika yote Mungu pekee ndiye atukuzwe.

Asante sana kwa kutumia muda wako kujifunza somo hili pamoja nami. Ninaamini kwamba kupitia makala hii umejifunza si tu umuhimu wa kushuhudia, bali pia umuhimu wa kuhakikisha kwamba kila ushuhuda tunaoutoa unamwakilisha Mungu kwa usahihi na unawajenga watu katika kweli ya Neno lake.

 Kama makala hii imekuwa baraka kwako, usisite kuishiriki na wengine ili nao wapate kujifunza.

 Kwa mafundisho na makala nyingine nyingi zaidi, ninakukaribisha kutembelea blogu yetu:

 [Victory In Christ](https://reference-url-citation.invalid/0)

 Mpaka wakati mwingine, 

Mungu akubariki sana.

Imeandaliwa na:

Samwel Ombeni

Victory In Christ.

Comments

Popular posts from this blog

JE MUIMBAJI WA PRAISE AND WORSHIP NI NANI?

Kutimia au Kubatilika kwa Unabii;