JE MUIMBAJI WA PRAISE AND WORSHIP NI NANI?
MUIMBAJI WA PRAISE AND WORSHIP NI NANI?
UTANGULIZI
Huduma ya Praise and Worship imekuwa sehemu muhimu sana katika ibada nyingi na hasa ibada za Kikristo. Hata hivyo, Watu wengi huiona huduma hii kama suala la kuimba pekee bila kufahamu wajibu, Sifa na maandalizi yanayohitajika kwa mtu anayehudumu katika eneo hili. Makala hii imeandaliwa ili kutusaidia kuelewa kwa kina maana ya Muimbaji wa Praise and Worship, sifa zake, Maandalizi anayopaswa kuwa nayo pamoja na tofauti kati ya kipaji na karama katika huduma.
• Katika makala hii tutajifunza:
• Maana ya Muimbaji wa Praise and Worship.
• Sifa za Muimbaji wa Praise and Worship.
• Maandalizi ya Muimbaji wa Praise and Worship kabla ya huduma.
• Tofauti kati ya Kipaji na Karama (kwa ufupi).
• Hitimisho.
MUIMBAJI WA PRAISE AND WORSHIP NI NANI?
Maana
Kabla ya kumjadili Muimbaji wa Praise and Worship, ni muhimu kwanza kumfahamu muimbaji kwa maana ya kawaida.
Muimbaji ni mtu anayejua kutumia sauti yake kwa mpangilio wa kimuziki, mara nyingi akiambatana na ala za muziki ili kufikisha ujumbe flani.
Uimbaji upo katika nyanja nyingi, mfano wa hizo ni;
• Uimbaji wa kitamaduni.
• Uimbaji wa kiinjili.
•Uimbaji wa choir.
• Uimbaji wa kidunia (Secular).
• Uimbaji wa sifa na kuabudu n.k.
Uimbaji ni nini?
Uimbaji ni kitendo au sanaa ya kutumia sauti kwa mpangilio wa melodi, mdundo na maneno kwa hali ya kuimbika na kufikisha ujumbe kwa jamii husika.
Ili uwe muimbaji lazima ujue kuhusisha mambo yafuatayo:-
(i) Sauti.
(ii) Mdundo.
(iii) Hisia.
(iv) Ujuzi katika matumizi ya ala za muziki.
(v) Ujumbe.
Katika hali ya kawaida watu huimba kwa sababu nyingi, mfano wa hizo ni:-
(i) Kujiburudisha.
(ii) Kuonesha hisia zao.
(iii) Kufariji.
(iv) Kufundisha.
(v) Kuwasilisha ujumbe.
Kusifu ni Nini?
Kusifu ni tendo la kutangaza ukuu, wema, nguvu, na matendo makuu ya Mungu kwa maneno, nyimbo, shangwe au matendo mengine ya kumheshimu. Kusifu mara nyingi huzingatia yale Mungu aliyotenda, anayoyatenda, na ahadi zake kwa watu wake.
Biblia inasema:
"Nitakushukuru, Ee Bwana, kwa moyo wangu wote; Nitayahubiri matendo yako yote ya ajabu." (Zaburi 9:1)
Pia:
"Ingieni malangoni mwake kwa kushukuru, Na nyua zake kwa kusifu." (Zaburi 100:4)
Na tena:
"Mkuu ndiye Bwana, mwenye kusifiwa sana; Wala ukuu wake hautafutikani." (Zaburi 145:3)
Maandiko haya yanaonyesha kwamba kusifu kunahusisha kutangaza matendo ya Mungu, wema wake, uaminifu wake, na ukuu wake kwa shukrani, furaha na heshima.
Kuabudu ni Nini?
Kuabudu ni tendo la kujinyenyekeza mbele za Mungu kwa kicho, heshima, upendo na kujitoa kwake kwa sababu ya yeye ni nani. Tofauti na kusifu, kuabudu huzingatia zaidi utakatifu, adhama, ukuu na uungu wa Mungu kuliko matendo yake pekee.
Yesu alisema:
"Lakini saa yaja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli; kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu." (Yohana 4:23)
Isaya Katika maono ya mbinguni tunaona viumbe wa mbinguni wakisema:
"Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu ni Bwana wa majeshi." (Isaya 6:3)
Na tena katika ufunuo biblia inasema..
"Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu Mwenyezi." (Ufunuo 4:8)
Maandiko haya yanaonyesha kwamba kuabudu ni mwitikio wa moyo unaomtambua Mungu kwa sababu ya yeye ni nani; yaani kwa utakatifu wake, adhama yake, ukuu wake na uungu wake.
Tofauti Kati ya Kusifu na Kuabudu
Kwa ufupi:
Kusifu humtangaza Mungu kwa yale aliyotenda, anayoyatenda, na kwa ukuu wake (Zaburi 150:2; Zaburi 145:3).
Kuabudu humheshimu Mungu kwa sababu ya yeye ni nani; kwa utakatifu, adhama na ukuu wake (Yohana 4:23–24).
Kusifu mara nyingi huambatana na shangwe na furaha (Zaburi 47:1).
Kuabudu mara nyingi huambatana na kicho, unyenyekevu na kujitoa (Waebrania 12:28).
Hata hivyo, kusifu na kuabudu si vitu vinavyopingana bali vinakamilishana katika maisha ya mwamini. Mara nyingi waamini huanza kwa kusifu, wakitangaza matendo na ukuu wa Mungu, na baadaye kuingia katika ibada ya kina zaidi wanapotafakari utakatifu, adhama na uwepo wake.
MUIMBAJI WA PRAISE AND WORSHIP NI NANI?
Ni mtu aliyeamua kujitoa ili atumike kufanya kazi ya Mungu kwa njia ya uimbaji.
Au;
Ni mtu anayemtumikia Mungu kwa njia ya uimbaji kwa kusudi la kuwaongoza watu katika sifa na kuabudu na kuandaa mazingira ya watu kuingia katika uwepo wa Mungu kupitia kusifu na kuabudu.
Muimbaji wa sifa na kuabudu si muimbaji wa kawaida tu, bali ni mtumishi halisi anayehudumu madhabahuni kwa nyimbo za sifa, nyimbo za kuabudu na hata wakati mwingine nyimbo za maombi, kwa lengo la kufanya ibada ikamilike na kumgusa Mungu kwenye kiti cha enzi.
Ikumbukwe kwamba Mungu hutamalaki katika sifa; hivyo ni muhimu sana waimbaji wajue kuwa wanafanya kazi njema ya kumfurahisha Mungu katika kiti Chake cha enzi. Mungu anapofurahi huwafikia watu wake kwa neema zake na kujibu mahitaji yao katika ibada.
Tukitazama Neno la MUNGU katika kitabu cha 1Mambo ya Nyakati 16:4-6
Hapa tunaona Daudi aliwateua watu maalumu kwa ajili ya kazi ya kumtukuza Mungu na kumshukuru Mungu.
Hapa tunajifunza kwamba ukitaka kuwa Muimbaji wa Praise and Worship lazima ukubali kujitoa kwa kusudi hilo na ukubali kwa moyo wako wote utumishi huo.
SIFA ZA MSINGI ZA MUIMBAJI WA PRAISE AND WORSHIP
(i) Ni mtumishi wa Madhabahuni
(ii) Ni mtu anayewaongoza watu kumwabudu Mungu Katika Roho na kweli;
Muimbaji wa Praise and worship huimba si kwa kuonekana au kwa kufurahisha wanadamu tu, bali katika Roho na kumwelekea Mungu.
Tukitazama neno hapa katika Yohana 4:23, tunajifunza kuwa MUNGU hupenda wamuabuduo katika Roho na kweli, na kwa msingi huo Muimbaji wa sifa na kuabudu anapaswa kujua yeye ni mmoja ya watu wenye kuwaongoza watu kumwabudu MUNGU kwa Roho na kweli.
(iii) Ni mtu mwenye moyo wa kupenda ibada.
(Anayependa ibada na kujinyenyekeza mbele za Mungu kila wakati).Sio kwa sababu umepangiwa kuja kuhudumu. Sio kwa sababu umepewa nafasi ya kuimba, basi ndiyo umebeba jukumu la kutimiza wajibu. Hapana!
Muimbaji wa Praise and Worship lazima awe na moyo wa kupenda ibada kuanzia ndani. Moyo wa kupenda ibada humfanya mtu kumtafuta Mungu kwa ajili Yake Mwenyewe na si kwa ajili ya kuonekana mbele za watu.
Tukitazama rejea nyingine katika:
Mathayo 15:8 inasema;
"Watu hawa waniheshimu kwa midomo yao, ila mioyo yao iko mbali nami." Tunachojifunza hapa kumbe kuna kumheshimu MUNGU kwa maneno yetu tu, lakini MUNGU yeye akitazama mioyo yetu tunakuwa tumejitenga mbali sana naye. Jambo hilo halimfurahishi MUNGU na humfanya MUNGU kukasirika na kuamua kumuacha Muimbaji afanye huduma kwa akili zake , sasa je MUNGU akituacha tutumie akili zetu bila ushirika nayeye tutaweza kumpendeza kweli?
Hivyo, Muimbaji wa Praise and Worship anatakiwa kuwa na moyo wa kupenda ibada kweli kweli, si kwa maneno tu bali kutoka ndani kabisa katika kilindi cha moyo.
Mungu huangalia moyo zaidi kuliko anavyoangalia mwonekano wa nje wa mtu. Hivyo ni muhimu kujua kuwa Mungu humjua kila mtumishi Wake aendaye mbele Zake hata kabla hajamweleza chochote, kwa maana Yeye huichunguza mioyo na kuijua kweli ya ndani ya mwanadamu.
(iv) Ni mtu anayeongozwa na Roho wa Mungu
Miongoni mwa sifa kuu za Muimbaji wa Praise and Worship ni kuongozwa na Roho Mtakatifu.
Roho Mtakatifu humwongoza mtu katika njia inayompendeza Mungu.
Ili uweze kuhudumu vizuri katika kundi la Praise and Worship na kuwa chombo kinachotumiwa kuandaa mazingira ya watu kuingia katika uwepo wa Mungu, ni lazima uwe unaongozwa na Roho Mtakatifu.
Roho Mtakatifu humsaidia Muimbaji wa Praise and Worship kufanya huduma yake iende kwa wepesi sana.
Roho Mtakatifu atakusaidia:-
(a) Kuongoza watu katika uwepo wa Mungu.
(b) Kugusa mioyo ya watu na kuwahudumia.
(c) Kuleta uwepo wa Mungu katika ibada.
(d) Kufungua vifungo vya watesi kwa watu wakati unaimba.
(e) Atatumia pumzi yako itokayo na maneno wakati unaimba na kubomoa makusudi ya adui na kuwaweka huru walioteswa na adui.
(f) Ni mtu anayejitakasa
Tatizo kubwa la waimbaji wengi ni kutokujitakasa.
Wengi wanafikiri kuwa kwa sababu wanaimba vizuri au wanatumika madhabahuni, basi hilo linatosha. Lakini Mungu hawaiti watumishi Wake kuwa na vipawa pekee, bali pia kuwa na maisha ya utakatifu.
Muimbaji wa Praise and Worship anapaswa kujitakasa katika mwenendo wake, maneno yake na matendo yake. Anatakiwa kujiepusha na dhambi na kila jambo linaloweza kuharibu ushirika wake na Mungu.
Neno la Mungu linasema:
"Bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote."
(1 Petro 1:15)
Daudi alikuwa mtu wa Mungu, lakini alipokosea alitubu na kutafuta kurejesha ushirika wake na Mungu. Hili linatufundisha kwamba Muimbaji wa Praise and Worship anatakiwa kuishi maisha ya toba na kujitakasa kila siku.
Utakatifu ni muhimu sana kwa mtu anayesimama mbele za Mungu na mbele za watu katika huduma.
(v) Awe mwenye nidhamu na anayependa kujifunza na kufundishika
Tatizo linguine kubwa kwa waimbaji wengi ni kutokutaka kujifunza na kufundishika. Wengi hufikiri kwamba kwa sababu wamekuwa wakiimba kwa muda mrefu, basi hawana tena kitu cha kujifunza.
Lakini haipaswi kuwa hivyo. Hata kama umeimba kwa miaka mingi, bado unahitaji kujifunza zaidi na kufundishika. Hata kama una kipawa kikubwa, ni muhimu kuendelea kupokea maelekezo, ushauri na mafundisho yatakayokusaidia kukua katika huduma.
Wakati mwingine unaweza kukuta mtu ana kipawa kikubwa sana cha uimbaji, lakini hana nidhamu ya kujifunza. Hali hiyo inaweza kuzuia ukuaji wake katika huduma.
Kujifunza ni jambo muhimu sana kwa kila Muimbaji wa Praise and Worship. Tunajifunza kila siku, na tunavyoendelea kujifunza ndivyo tunavyoendelea kukua zaidi katika huduma.
Ukiendelea kusoma m1 Mambo ya Nyakati 25:7
Hapa tunaona kwamba wale waliokuwa wakihudumu katika huduma hii ya kumsifu MUNGU walifundishwa na kupewa maelekezo ili waweze kumtumikia Mungu kwa usahihi.
Jambo lingine ambalo ni muhimu kuliona hap ani hili, Idadi ya kundi lote waliokubali kukaa pamoja na kujifunza pamoja ilikuwa ni watu 288 jambo ambalo kwa nyakati hizi kupata watu waliojitoa kwa idadi kubwa namna hii si rahisi sana.
Kwahiyo kujifunza na kufundishika kila leo ni muhimu sana.
Tuajifuza somo jingine vilevile ya kwamba Kuwa na kipawa cha uimbaji ni muhimu, lakini Mazoezi au kujifunza ni muhimu zaidi.
Huduma pia inahitaji kuandaliwa vema na maandalizi hayawezi kufanywa na mtu mmoja mmoja pekee, lazima kuna wakati wa kukaa kupangana na kuelekezana na kupata muelekeo mmoja utakaofanya huduma iende kwa utaratibu mzuri na unaoleta matokeo mazuri.
(vi) Muimbaji awe anaimba kwa lengo la kumtukuza Mungu na si kujitafutia sifa.
Hili ni jambo muhimu sana kwa kila Muimbaji wa Praise and Worship kulifahamu na kulizingatia.
Lakini wakati mwingine baada ya huduma watu huweza kukufuata na kukuambia:
"Mtumishi, leo mmeimba vizuri sana, hongereni sana."
Swali la kujiuliza ni hili:
Je, utajibuje?
Watu wengi hujibu kwa namna mbalimbali kama vile:-
"Utukufu kwa Yesu."
"Ni neema ya Mungu."
"Usinishukuru mimi, mshukuru Yesu."
"Mungu ndiye ametenda."
"Usinipe utukufu mimi, wewe mpe Yesu."
Majibu hayo si mabaya. Hata hivyo, wakati mwingine yanaweza kuacha tafsiri tofauti katika mioyo ya watu wanaotoa pongezi hizo.
Kumbuka kuwa wengine wanaweza kufasiri majibu hayo kama vile hujathamini kile walichokisema. Wengine wanaweza kuhisi kana kwamba umepuuza kile walichokiona katika huduma yako.
Kwa hiyo Muimbaji wa Praise and Worship anatakiwa kuwa makini katika namna anavyojibu pongezi anazopewa.
Biblia pia inaonyesha mifano ya watu waliopongezwa kwa kazi nzuri walizozifanya.
Katika 1 Wakorintho 16:17-18, Mtume Paulo aliwapongeza Stefano, Fortunato na Akaiko kwa mchango wao katika huduma.
Vilevile katika Wafilipi 2:19-20, Paulo alimpongeza Timotheo kwa uaminifu wake na moyo wake wa kuwajali watu wa Mungu.
Pia katika Mathayo 25:21, tunamwona Bwana akisema:
"Vema, mtumwa mwema na mwaminifu."
Kwa hiyo tunaona kuwa kupongezwa si jambo baya.
Jambo la muhimu ni namna mtu anavyopokea pongezi hizo na namna anavyoendelea kubaki mnyenyekevu mbele za Mungu.
Mifano ya majibu mazuri ambayo yanaweza kutolewa ni kama:-
•"Asante; tunashukuru sana."
•"Ahsante sana kwa pongezi; tunamshukuru Mungu kwa kutusaidia."
•"Tunashukuru; endelea kutuombea."
•"Tunashukuru; Mungu ametenda."
•"Asante kwa kutambua kile Mungu anachofanya."
•"Tunashukuru; ni Mungu ametuwezesha kuyatenda hayo."
•"Ahsante kwa pongezi na muendelee kutuinua katika maombi."
Majibu mazuri kama hayo hujenga mahusiano mazuri na watu na huonyesha tabia njema ya mtumishi wa Mungu.
Kupitia majibu yako mazuri utawavutia wengi pia katika huduma yako na kuwafaidia wengine.
Lakini pia lazima ujue kuwa majibu mazuri yanaweza kukupa kibali kwa watu, maana usemi wa mtu huweza kumpa aina fulani ya kibali machoni pa watu.
Pamoja na hayo yote, Muimbaji wa Praise and Worship anatakiwa kujilinda dhidi ya tamaa ya kutafuta sifa kutoka kwa wanadamu.
Anapoanza kuimba kwa kusudi la kupongezwa, kujulikana au kusifiwa na watu, anaweza kuingia katika hatari ya:
•Kiburi.
•Kujisifu.
•Kujionyesha.
•Kufanya mambo ili kuonekana.
•Kumsahau Mungu.
•Kuwakatisha wengine tamaa.
Ni muhimu kukumbuka kuwa kila kipawa, uwezo na neema ya kuhudumu hutoka kwa Mungu.
Hakuna mtu anayepaswa kujivunia kipawa chake kana kwamba amekipata kwa nguvu zake mwenyewe.
Kwahiyo natamani sana tujue kuwa lengo kuu la Muimbaji wa Praise and Worship ni kumtukuza Mungu, kuifanya mbingu ifurahi na kushuka kukutana na watu Wake katika ibada.
(vii) Awe mnyenyekevu
Tukumbuke Neno la Mungu linasema:
"Mungu huwapinga wenye kiburi, bali huwapa neema wanyenyekevu." (1petro 5;5)
Muimbaji wa Praise and Worship anatakiwa kukubali kwamba kila neema aliyopewa imetoka kwa Mungu. Kadiri Mungu anavyozidi kumuinua katika huduma, ndivyo anavyopaswa kuzidi kuwa mnyenyekevu.
Kama Muimbaji hatakuwa makini, anaweza kuanza:
Kutafuta sifa za wanadamu.
Kujiona bora kuliko wengine.
Kushindana madhabahuni.
Kutafuta umaarufu na kujulikana zaidi kuliko huduma yenyewe.
Mambo hayo yanaweza kuonekana madogo mwanzoni, lakini baadaye yanaweza kuharibu huduma ya uimbaji na kuondoa kusudi halisi la kumtumikia Mungu.
(viii) Awe na kipawa cha uimbaji na awe mwenye kupenda kufundishika
Watu wengi hujivunia kipawa walichonacho cha uimbaji. Ni kweli kwamba kipawa ni muhimu katika huduma ya Praise and Worship, lakini kipawa pekee hakitoshi kumfanya mtu kuwa Muimbaji bora.
Mtu anaweza kuwa na kipawa kikubwa cha kuimba, lakini bado akahitaji kufundishwa, kuelekezwa na kuongozwa ili aweze kukua katika huduma.
Kipawa ni msingi mzuri wa kuanzia, lakini maendeleo ya huduma hutegemea pia utayari wa mtu kujifunza na kufundishika.
Sasa jiulize:
Je, una kipawa cha kuimba tu, au pia una moyo wa kujifunza?
Wapo watu wengi wenye vipaji vikubwa sana, lakini kwa sababu hawataki kufundishwa au kuelekezwa, hushindwa kufikia kiwango walichoweza kufika katika huduma.
Vipaji vyao huwa vikubwa, lakini ukuaji wao huwa mdogo kwa sababu hawakubali kufundishika.
Kufundishika humsaidia mtu:
•Kuboresha uwezo wake.
•Kurekebisha makosa yake.
•Kupanua ufahamu wake wa huduma.
•Kukua kiroho na kimatumizi.
Ni muhimu kukumbuka kuwa:
Kipaji ni muhimu, lakini mazoezi ni muhimu zaidi.
Hata hivyo, mazoezi peke yake hayatoshi. Lazima kuwe na mtu wa kukuongoza, kukusikiliza, kukushauri na kukurekebisha pale inapobidi.
Hapo ndipo mtu hujengwa na kuwa Muimbaji bora zaidi.
Soma: 1 Mambo ya Nyakati 25 utajifunza mengi Zaidi.
(ix) Awe mtu anayeheshimu madhabahu na kuepuka kuchanganya madhabahu.
Muimbaji wa Praise and Worship anatakiwa kuelewa kuwa si kila madhabahu ni madhabahu ya Mungu.
Kila madhabahu ina msingi wake, maono yake, taratibu zake na mwelekeo wake wa kiutumishi. Hivyo ni muhimu kwa Muimbaji kujua mahali anapohudumu na madhabahu anayoisimamia.
Katika Biblia tunaona mfano wa Eliya na manabii wa Baali. Wote walikuwa na madhabahu zao, lakini Mungu alijibu madhabahu ya Eliya pekee. Madhabahu ya Baali haikupata majibu yoyote.
Hii inatufundisha kuwa si kila madhabahu inayotajwa kwa jina la ibada au Imani ya kikristo ina kibali cha Mungu.
Muimbaji wa Praise and Worship anatakiwa kuwa mwangalifu sana asichanganye madhabahu ya Mungu na madhabahu ambazo hazina msingi wa Mungu.
Kuchanganya madhabahu kunaweza kuharibu huduma ya mtu, kuharibu ushirika wake na Mungu na hata kumtoa katika mwelekeo ambao Mungu alimkusudia.
Neno la Mungu pia linatuonya kuwa si kila anayesema:
"Bwana, Bwana.. ataingia katika Ufalme wa Mungu."
Wapo watakaodai walifanya mambo mengi kwa jina la Mungu, lakini hawakutembea katika mapenzi Yake.
Kwa hiyo Muimbaji wa Praise and Worship anatakiwa kuwa na utambuzi wa kiroho, kujua anahudumu wapi, anashirikiana na nani, na madhabahu anayoisimamia ina msingi gani.
Madhabahu ya Mungu inapaswa kuheshimiwa, kulindwa na kutunzwa katika usafi wake hasa kiroho.
Kuepuka kuchanganya madhabahu ni sehemu ya hekima, utii na uaminifu kwa Mungu aliyekuita katika huduma.
(x) Awe msomaji wa Neno la Mungu.
Neno la Mungu ni chakula cha kiroho kwa kila mtumishi wa Mungu.
Muimbaji wa Praise and Worship anatakiwa kuwa msomaji wa Neno la Mungu ili aendelee kukua kiroho na kuongeza ufahamu wake.
Faida za kujifunza Neno la Mungu ni nyingi, zikiwemo:
• Kukuza ufahamu wa kiroho.
• Kujenga imani.
• Hukupa ufahamu wa namna ya kuenenda katika Maisha ya kawaida na huduma.
• Kumsaidia Muimbaji kuwaongoza watu kwa ufahamu sahihi wa Mungu.
Muimbaji anayelisoma Neno la Mungu kwa bidii huwa na msingi mzuri wa kumjua Mungu na kuhudumu kwa hekima zaidi.
(xi) Akubali kuwa yeye ni mtumishi wa Mungu na si kama msanii wa jukwaani.
Muimbaji wa Praise and Worship anatakiwa kutambua kwamba yeye ni mtumishi wa Mungu kwanza kabla hajawa muimbaji. Na kwahiyo anatakiwa kuwa muangalifu sana hata namna anavyohudumu madhabahuni.
Vile vile anavyoimba vitedo anavyo vionyesha wakati anaimba vinaweza kumtofautisha au kumlinganisha na wasanii wa kidunia. Kumbuka muimbaji awapo madhabahuni sio msanii ni Mtumishi mtoa huduma, tena huduma ya kuhudumia mioyo ya watu na kuwafanya watu wakutane na MUNGU kwa njia hiyo ya uimbaji
Huduma yake si kwa ajili ya kujionyesha, kutafuta umaarufu au kujenga jina lake mwenyewe, bali ni kwa ajili ya kumtukuza Mungu na kuwahudumia watu Wake.
Anaposimama madhabahuni anatakiwa kujiona kama mtumishi aliyebeba wajibu wa kuwasaidia watu kumkaribia Mungu.
Kwa hiyo Muimbaji wa Praise and Worship hapaswi kujiona kama msanii wa jukwaani tu, bali kama mtumishi aliyeitwa na Mungu kwa kusudi maalumu.
MAANDALIZI YA MUIMBAJI WA PRAISE AND WORSHIP KABLA YA HUDUMA
Kumwimbia Mungu si kuwa na sauti nzuri na ya kuvutia tu. Ili mtu awe Muimbaji kamili na mwenye uwezo wa kumtumikia Mungu, lazima awe ameandaliwa na kutengenezwa ili autimize wito wake kwa ufanisi.
Utumishi haujengwi kwa siku moja wala kwa muda mfupi. Maandalizi na matengenezo ya mtumishi ni hatua kwa hatua na huendelea kadiri mtu anavyozidi kukua katika huduma.
Sasa jiulize:
Je, uko tayari kupokea marekebisho hayo ili ufae kuwa chombo cha Mungu?
Wengine hudhani kwamba uimbaji ni kuitikia na kukariri maneno ya nyimbo tu. Lakini ukweli ni kwamba huduma ya Praise and Worship ni zaidi ya hapo.
Kama ilivyo kwa watumishi wengine wa Mungu, waimbaji pia hukutana na majaribu mbalimbali katika maisha na huduma zao.
Kuyashinda majaribu hayo ni sehemu ya ukuaji wa kiroho na ukomavu katika huduma. Lakini majaribu yasiposhughulikiwa vizuri yanaweza kuathiri huduma, mwenendo na hata wito wa mtumishi wa Mungu.
Ndiyo maana ni muhimu Muimbaji wa Praise and Worship kujengwa katika misingi imara itakayomsaidia kusimama katika huduma yake.
Miongoni mwa mambo muhimu ya kuzingatia ni haya yafuatayo:
(i) Awe na maisha ya utakatifu
Utakatifu ni msingi muhimu sana kwa Muimbaji wa Praise and Worship.
Neno la Mungu linasema:
1 Petro 1:15-16
"Bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu."
Maisha ya utakatifu humsaidia mtumishi kuwa karibu na Mungu na kulinda ushirika wake na Bwana.
Maandiko mengine ya kujifunza kuhusu utakatifu ni:
Walawi 20:7
Walawi 19:2
Walawi 11:44
Waebrania 12:14
1 Wathesalonike 4:3-4
2 Wakorintho 7:1
2 Timotheo 2:19-21
Muimbaji wa Praise and Worship anatakiwa kujitahidi kuishi maisha yanayompendeza Mungu, kwa sababu huduma yenye nguvu hujengwa juu ya msingi wa ushirika mzuri na Mungu.
(ii) Awe mwenye nidhamu na utii
Katika mwili wa Kristo na katika huduma za Mungu, tunakutana na viongozi wa aina mbalimbali.
Wakati mwingine unaweza kujikuta unaongozwa na mtu mwenye umri mdogo kuliko wewe au mwenye uzoefu mdogo kuliko unaodhani unao.
Hata hivyo, ili huduma iende vizuri ni muhimu kujifunza kutii mamlaka yaliyowekwa na Mungu.
Muimbaji wa Praise and Worship anatakiwa kujifunza si kuongoza tu, bali pia kuongozwa.
Anatakiwa kukubali maelekezo na ratiba za huduma bila malalamiko yasiyo ya lazima.
Pia anatakiwa kukubali kurekebishwa pale anapokosea.
Ukikosea sauti, ukikosea maneno ya wimbo au ukikosea katika utendaji wa huduma, kubali kurekebishwa ili uzidi kukua.
Nidhamu nzuri huonekana pia katika mambo yafuatayo:
• Muimbaji mzuri:
• Huhudhuria mazoezi.
• Huheshimu viongozi.
• Huheshimu muda wa ibada.
• Hufuata maelekezo ya huduma.
• Hukubali kusahihishwa pale inapobidi.
Pasipo nidhamu, ni vigumu sana kujenga huduma imara na yenye kuaminika.
(iii) Awe na ushirika mzuri na Roho Mtakatifu ili aweze kuhudumia watu wa Mungu
Huduma ya Praise and Worship ni huduma ya kiroho. Kwa sababu hiyo, Muimbaji wa Praise and Worship anatakiwa kuwa na ushirika mzuri na Roho Mtakatifu ili aweze kutekeleza huduma yake kwa ufanisi.
Roho Mtakatifu humsaidia mtumishi katika maeneo mbalimbali ya huduma.
Miongoni mwa mambo ambayo Roho Mtakatifu humsaidia Muimbaji ni:
• Kuchagua nyimbo sahihi.
• Kuongoza ibada kwa ufasaha.
• Kugusa mioyo ya watu wanaohudumiwa.
• Kusaidia watu kuingia katika uwepo wa Mungu.
• Kuelekeza mtiririko wa ibada kadiri Mungu anavyotaka.
Kadiri ushirika wa mtu na Roho Mtakatifu unavyozidi kuimarika, ndivyo huduma yake inavyozidi kuwa na matokeo mazuri kwa watu wa Mungu.
(iv) Awe mnyenyekevu
Unyenyekevu ni sifa muhimu sana kwa Muimbaji wa Praise and Worship.
Kutokuwa mnyenyekevu kunaweza kuzaa kiburi, majivuno na kujiona kuwa bora kuliko wengine.
Muimbaji mzuri anatakiwa kujifunza kubaki mnyenyekevu hata pale anapotumiwa sana na Mungu, anapopongezwa au anapoonekana kuwa na mafanikio makubwa katika huduma.
Mtu anapokuwa mnyenyekevu huwa rahisi kufundishika, kurekebishika na kuendelea kukua katika huduma.
Kumbuka kwamba kila kipawa, kila uwezo na kila mafanikio katika huduma hutoka kwa Mungu.
Kwa hiyo, Muimbaji wa Praise and Worship anatakiwa kujifunza kumtegemea Mungu na kubaki mnyenyekevu mbele Zake na mbele za watu.
Tofauti kati ya Kipaji na Karama
Kipaji ni uwezo wa asili ambao mtu anaweza kuzaliwa nao au kuukuza kwa mazoezi na juhudi binafsi.
Karama ni uwezo au neema maalumu inayotolewa na Mungu kwa kusudi la kuwahudumia watu na kulijenga Kanisa kupitia kazi ya Roho Mtakatifu.
Ingawa mara nyingi kipaji na karama vinaweza kufanya kazi pamoja, si kila kipaji ni karama, na si kila karama hutegemea kipaji cha asili."
HITIMISHO
Baada ya kujifunza mada hii, ni wazi kuwa Muimbaji wa Praise and Worship si mtu anayejua kuimba tu, bali ni mtumishi wa Mungu mwenye wito wa kuwasaidia watu kuingia katika uwepo wa Mungu kupitia sifa na ibada.
Tumeeleza sifa mbalimbali zinazopaswa kuonekana katika maisha ya muimbaji wa Praise and Worship, pamoja na maandalizi muhimu yanayomwezesha kuhudumu kwa ufanisi na kwa kumpendeza Mungu. Mambo haya hayakusudiwi kuwakatisha tamaa wale wanaotamani kuhudumu, bali kuwasaidia kuelewa ukubwa wa jukumu waliloitiwa.
Sasa ni wakati wa kila msomaji kujiuliza maswali haya muhimu:
Je, mimi ninayejiita muimbaji wa Praise and Worship ninaishi maisha yanayompendeza Mungu?
Je, ninahudumu kwa kusudi la kumtukuza Mungu au kutafuta sifa za wanadamu?
Je, ninaheshimu madhabahu ya Mungu na kuishi katika utii wa Neno Lake?
Je, ninajitahidi kukua kiroho, kujifunza na kufundishika ili niwe chombo bora zaidi katika huduma?
Majibu ya maswali haya yatamsaidia kila mmoja kutathmini nafasi yake mbele za Mungu na kufanya marekebisho pale yanapohitajika.
Mwisho,
Tukumbuke kuwa Mungu hatazami sauti nzuri pekee, umahiri wa muziki pekee, wala umaarufu wa mhudumu. Mungu huutazama moyo wa mtu anayehudumu mbele Zake.
Hivyo basi, ikiwa unatamani kuwa Muimbaji wa Praise and Worship anayempendeza Mungu, jitahidi kuishi maisha ya utakatifu, unyenyekevu, utii na kujitoa kwa Mungu. Ruhusu Roho Mtakatifu akuongoze kila siku, ili huduma yako isiwe baraka kwa watu pekee, bali pia iwe sadaka yenye harufu nzuri mbele za Mungu.
Mungu akubariki unapomtumikia katika huduma ya kusifu na kuabudu.
Imetayarishwa na:
SAMWEL OMBENI
Mwandishi wa Makala.
.png)
Comments
Post a Comment